VIDEO: Miujiza ya Taifa Stars na matukio yaliyotikisa michezo 2009-2019

Muktasari:

Yapo matukio mengi ya kimichezo ambayo yatatokea katika kipindi cha miaka 10 ijayo lakini pia kuna rekodi kadhaa ama zitawekwa, kufikiwa au kuvunjwa. Pia wapo watu binafsi au timu ambazo zitafanya mambo ya kipekee yatakayoacha historia wapo ambao watavurunda

Tumeingia mwaka mpya wa 2020 lakini ni mwanzo wa muongo mpya baada ya miaka 10 kupita kuanzia mwaka 2009 hadi 2019.
Yapo matukio mengi ya kimichezo ambayo yatatokea katika kipindi cha miaka 10 ijayo lakini pia kuna rekodi kadhaa ama zitawekwa, kufikiwa au kuvunjwa. Pia wapo watu binafsi au timu ambazo zitafanya mambo ya kipekee yatakayoacha historia wapo ambao watavurunda.
Wakati tukianza muongo mwingine, haya ni matukio mbalimbali yaliyotokea katika kipindi cha miaka 10 iliyopita na dondoo za watu, timu au wadau wa waliotamba na hata kumbukumbu zisizovutia ambazo zimetokea katika muongo uliopita.

Mbwana Samatta
Hapana shaka nahodha wa timu ya Taifa ya Tanzania ‘Taifa Stars’, Mbwana Samatta ndiye mwanamichezo aliyefanya vizuri kuliko mwingine katika muongo uliopita.
Akiwa na TP Mazembe alinyanyua taji la Ligi ya Mabingwa Afrika 2015, mwaka ambao alikuwa mfungaji bora wa mashindano hayo katika kipindi hicho cha miaka 10, Samatta ameshinda mataji manne ya Ligi Kuu ya DR Congo na mataji mawili ya ngao nchini humo.
Ameshinda taji la Ligi Kuu ya Ubelgiji msimu wa 2018/2019 na ubingwa Super Cup Ubelgiji mwaka 2019 akiwa na Genk. Ameshinda tuzo ya mchezaji bora Afrika anayecheza ndani mwaka 2015, alikuwemo katika kikosi bora cha Afrika na ameshinda tuzo ya mchezaji bora wa Ubelgiji mwenye asili ya Afrika mwaka jana.

Simba
Katika kipindi cha miaka 10 iliyopita Simba ndio klabu ya soka iliyofanikiwa kulinganisha na nyingine.
Imetinga hatua ya robo fainali ya Ligi ya Mabingwa Afrika mara moja msimu wa 2018/2019, imetwaa Kombe la Ligi Kuu Tanzania Bara mara nne, Kombe la Mapinduzi mara mbili na Ngao ya Jamii mara tano.
Yanga inafuata imeshiriki hatua ya makundi ya Kombe la Shirikisho Afrika mara mbili, mwaka 2016 na 2018, imetwaa ubingwa wa Ligi Kuu mara tano na imechukua Kombe la Klabu Bingwa Afrika Mashariki na Kati (Kombe la Kagame) mara mbili.

‘Hat-trick’ za Tambwe
Rekodi ya mshambuliaji raia wa Burundi, Amissi Tambwe ya kuwa kinara wa kufunga mabao matatu katika mchezo mmoja ‘hat-trick’ mara nyingi katika Ligi Kuu Tanzania Bara ndani ya muongo uliopita huenda ikawa mlima mrefu kuupanda kwa wachezaji wengine miaka ijayo.
Tambwe amefunga mabao matatu au zaidi katika mchezo mmoja mara sita katika Ligi Kuu na hakuna mchezaji aliyewahi kufanya hivyo nchini.
Alianza kufunga ‘hat trick’ ya kwanza Septemba 18, 2013 akiwa Simba na kuibuka na ushindi wa mabao 6-0 dhidi ya Mgambo JKT akipachika wavuni mabao manne. Alifunga  Februari Mosi 2014 mabao matatu akiiongoza Simba kuichapa Oljoro JKT 4-0 na akafunga nyingine dhidi ya Coastal Union Aprili 8,2015 ambapo alifumania nyavu mara tano. Wakati huo akiwa Yanga.
Desemba 19,2015 alifunga Yanga ilipoichapa Stand United mabao 4-0, akafunga tena akiiongoza Yanga kuichapa Majimaji 5-0 Januari 21,2016
Pia alifunga mabao matatu katika ushindi wa 4-0 ambao Yanga ilipata dhidi ya Polisi Moro Aprili 27, 2015.

Taifa Stars yafuzu Afcon, Chan
Katika kipindi hicho cha miaka 10 iliyopita, Taifa Stars ilivunja mwiko wa kutoshiriki Fainali za Mataifa ya Afrika (Afcon) kwa miaka 39 baada ya kushiriki nchini Misri mwaka jana na kushika mkia katika hatua ya makundi.
Kana kwamba haitoshi mwaka 2009 kushiriki Fainali za Mataifa ya Afrika kwa Wachezaji wanaocheza Ligi za Ndani (Chan). Taifa Stars ilikata tiketi hiyo baada ya kuilaza Sudan katika mchezo uliochezwa ugenini jijini Khartoum.

Taifa Stars, Mwakinyo watinga Ikulu
Ukiachana na Rais wa awamu ya nne, Jakaya Kikwete ambaye enzi za utawala wake aliwaalika wanamichezo mbalimbali Ikulu na kula nao chakula, John Magufuli  naye ameendeleza utaratibu huo huku bahati ya kwanza ikiwaangukia wachezaji wa Taifa Stars na bondia Hassan Mwakinyo.
Nyota wa Taifa Stars walikuwa wanamichezo wa kwanza kualikwa Ikulu na Rais Magufuli na Mwakinyo ambapo alikula nao chakula na kuwapa zawadi ya viwanja kila mmoja mkoani Dodoma kufuatia kufanya vizuri kimataifa Taifa Stars ikiwa imefuzu Afcon kwa mara ya pili baada ya ile ya 1980.
Mwakinyo alialikwa baada ya ushindi wa TKO raundi ya tano  dhidi ya Eduardo Gonzalez wa Argentina katika pambano la kimataifa lililopigwa nchini Kenya, awali bondia huyo aliyeibuliwa na promota Hassan Mwanzoa alimchapa Sam Eggington wa Uingereza pambano lililompa umaarufu.

Obama apigia debe kikapu
Rais mstaafu wa Marekani, Barack Obama atakumbukwa katika kipindi cha miongo 10 wenye tasnia ya michezo baada ya kupigia chapuo kuanzishwa Ligi ya Mpira wa Kikapu Afrika  ambayo tayari imeanza na Tanzania ilikuwa miongoni mwa nchi zilizoshiriki hatua za awali za kutafuta tiketi ya kufuzu licha ya klabu ya JKT kuondoshwa kwenye raundi ya pili.

Ngumi
Uendeshaji wa ngumi za kulipwa nchini uliingia kwenye mabadiliko ya mfumo kutoka kuongozwa na vyama vingi na tangu Machi 30, 2019  mchezo huo unaongozwa na Kamisheni ya TPBRC. Uchaguzi mkuu wa kwanza wa kamisheni ulimchagua Joe Anea kuwa rais wa kwanza wa TPBRC, baada ya wadau wa ngumi kuachana na mfumo wa vyama vingi  vya TPBC, TPBC Limited, TPBO na TPBL na PST.

Riadha kimataifa yarejea
Ulikuwa muongo wa wanariadha nchini ambao mbali na medali ya shaba iliyotwaliwa na Alphonce Simbu kwenye mashindano ya dunia ya 2017 na ile ya Francis Damiano katika michuano ya vijana ya Jumuiya ya Madola, mwamko ulikuwa mkubwa kwa wanariadha kutwaa medali za kimataifa.
Simbu alitwaa medali ya dhahabu ya Mubai Marathoni, Failuna Abdi shaba katika mbio za Haspa Hambarg Marathoni Ujerumani, Agostino Sulle alivunja rekodi ya Taifa ya marathoni kwenye mbio za Toronto nchini Canada alipotwaa medali ya fedha.

Mtanzania achezesha kombe la dunia
Mwamuzi Karim Zulficar wa Tanzania naye aliingia kwenye historia kwa kuwa miongoni mwa Waafrika wawili walioteuliwa kuchezesha kombe la dunia la mpira wa kikapu  nchini China mwaka jana.

Mtanzania atema kilinda ulimi ulingoni
Kipigo cha TKO kwa bondia Selemani Bangaiza nchini Australia kiliibua mjadala baada ya video ya pambano lake dhidi ya mwenyeji Andrew Moloney kuonyesha akisalimu amri na kutema kilinda ulimi ‘gurmsheet’  bila kupigwa.
Inadaiwa bondia huyo alicheza mchezo mchafu kwa lengo la kujipatia fedha na hakuwa na dhamira ya kushindana dhidi ya mpinzani wake.
Waziri wa Habari, Sanaa, Utamaduni na Michezo Dk Harrison Mwakyembe aliagiza bondia huyo afungiwe.

Baraka mfungaji bora kikapu Afrika
Baraka Athumani ameingia katika kumbukumbu nzuri kwa kuwa mfungaji bora wa mashindano ya mpira wa kikapu ya Afrika kanda licha ya timu ya Taifa kuondoshwa mapema baada ya kufungwa mechi zote za makundi.
Katika mashindano hayo, Baraka alionyesha kiwango cha juu kiasi cha kuzivutia timu mbalimbali zilizoshiriki ambazo zilianza mchakato wa kutaka kumsajili baada ya kumalizika mashindano hayo.
Kitendo cha Baraka kucheza kwa ufanisi mashindano kilikumbusha enzi za kina Abdallah Ramadhani ‘Dulla’ aliyewahi kutamba na klabu ya Pazi

Tanzania yachemka Olimpiki, Madola
Ulikuwa muongo mgumu kwa timu za Tanzania kwenye michezo ya Olimpiki 2016 kule Rio de Janeiro, Brazil, michezo ya madola Australia mwaka 2018 na michezo ya Afrika kule Morocco mwaka 2019 ambapo timu za Tanzania za riadha, judo na tenisi ya meza ziliondoshwa mapema mashindanoni katika michezo yote.
Licha ya Simbu kuingia tano bora kwenye Olimpiki ya Rio 2016, Watanzania wengine walishindwa kufurukuta na kuambulia kushiriki.

Vigogo BMT waondolewa
Alianza Henry Lihaya ambaye alikuwa Katibu Mkuu wa Baraza la Michezo la Taifa (BMT) kuondolewa katika nafasi hiyo na nafasi yake kuchukuliwa na Mohammed Kiganja ambaye baadaye alihamishiwa Ofisi ya Waziri Mkuu kuwa Mkurugenzi wa Sherehe na Maadhimisho ya Taifa na Alex Nkenyenge kukaimu nafasi yake BMT.
Nkenyenge  naye hakudumu na kuondolewa na nafasi hiyo sasa inakaimiwa na Neema Msitha tangu Julai 7, mwaka jana.

Pambano layeyukia ukumbini
Pambano la ubingwa wa UBO kati ya bondia Mtanzania Twaha Kiduku na Tshibangu Kayembe wa DR Congo liliyeyukia ukumbini baada ya vurugu kutokea na mabondia hao kutopigana. Kitendo hicho kilisababisha Kamisheni ya Ngumi za Kulipwa Tanzania (TPBRC) kumfungia promota wa pambano hilo Kaike Siraju.

Tanzania yatia aibu michezo ya Afrika
Tukio hili linaingia kwenye historia ya muongo mmoja kwa kwa kikosi cha riadha cha Tanzania kushinda bila kula kwa kutokuwa na fedha za kigeni walipokuwa Cairo, Misri wakisubiri kuunganisha ndege kwenda Morocco  kwenye michezo ya Afrika Mwaka jana.
Meneja wa timu hiyo Donati Masawe alisema mbali na kukosa fedha za kununulia chakula Misri walipokaa kwa saa nane, hata sare za kimichezo haikupewa ingawa Naibu Waziri wa Habari, Sanaa, Utamaduni na Michezo, Juliana Shonza alikanusha kukosa sare hizo huku akieleza kutofahamu kama walishinda njaa kwa kukosa fedha.
Hiyo ilikuwa mara ya pili kwa timu ya Tanzania kukutana na fedheha kwenye michezo ya Afrika, awali ilikuwa mwaka 2011 ambapo aliyekuwa kocha wa timu ya Taifa ya ngumi, Pimenter Hurtado alilalamika timu hiyo kuazima jezi za michezo kwa timu ya Zambia baada ya kutopewa wakati wakiondoka nchi kwenda Msumbiji katika michezo hiyo.
Mwaka 2011 timu ya Taifa ya netiboli ‘Taifa Queens’ ilitwaa medali ya fedha kwenye mashindano hayo, ingawa mchezo huo umeporomoka na mwaka jana walishindwa kushiriki mashindano ya Afrika nchini Afrika Kusini dakika za mwishoni kutokana na ukata.
Kitendo cha timu hiyo kushindwa kushiriki mashindano hayo kiliibua mjadala na baadhi ya wadau waliutaka uongozi wa Chama cha Netiboli Tanzania (Chaneta) kujitafakari.

Gidabuday abwaga manyanga RT
Aliyekuwa Katibu Mkuu wa Riadha Tanzania, Wilhelim Gidabuday alitangaza kujiuzulu nafasi hiyo kwa kile ambacho alieleza kupisha maslahi mapana ya riadha nchini na nafasi yake kukaimiwa na Ombeni Zavalla ingawa rais wa RT Anthony Mtaka amesema nafasi hiyo itakuwa ya kuajiriwa.
Gidabuday alifikia uamuzi huo baada ya kutokea msuguano wa mara kwa mara na uongozi wa juu ndani ya taasisi hiyo kabla ya kuamua kuachia ngazi.

Mufuruki akumbukwa gofu
Familia ya wachezaji gofu ilipata pigo kufuatia kifo cha mmoja wa wadau wakubwa wa mchezo huo nchini bilionea Ali Mufuruki aliyefariki dunia nchini Afrika Kusini  mwaka jana.
Mwenyekiti wa Chama cha Gofu Tanzania (TGU), Chris Martin akimueleza Mufuruki namna alivyokuwa amepanga kujenga uwanja wa gofu katika hifadhi ya Saadan enzi za uhai wake. Mufuruki alikuwa nembo ya mchezo wa gofu kutokana na umahiri wake katika mchezo huo ambao alitilia mkazo.