Scholes ahofia Pogba, Rashford kusepa Manchester United

Muktasari:

Mbappe ameshafunga mabao  20 kwenye Ligi ya Mabingwa Ulaya, lakini Marcus anacheza kwenye Europa League. Hivyo atahitaji sana na yeye kucheza kwenye Ligi ya Mabingwa Ulaya

MANCHESTER, ENGLAND.GWIJI wa Manchester United, Paul Scholes ameibua wasiwasi wake kwamba Marcus Rashford na Paul Pogba wataihama timu hiyo kama itashindwa kufuzu kucheza kwenye Ligi ya Mabingwa Ulaya msimu ujao.
Kikosi hicho cha kocha Ole Gunnar Solskjaer kinamaliza mwaka 2019 kikiwa kwenye nafasi ya tano katika msimamo wa Ligi Kuu England, pointi nne nyuma ya timu inayoshika  nafasi ya nne,  Chelsea baada ya ushindi wao wa  2-0 dhidi ya Burnley  Jumamosi iliyopita. Straika  Rashford ameendelea kucheza kwenye ubora mkubwa akifikisha mabao 12 kwenye ligi hiyo msimu huu na kumfannya Scholes aanze kumlinganisha na staa wa Paris Saint-Germain, Kylian Mbappe.
“Kuna kitu wanafanana. Mbappe ameshafunga mabao  20 kwenye Ligi ya Mabingwa Ulaya, lakini Marcus anacheza kwenye Europa League. Hivyo atahitaji sana na yeye kucheza kwenye Ligi ya Mabingwa Ulaya,” alisema Scholes.
“Hakuna namna, Man United wanahitaji kucheza kwenye michuano hiyo ya Ulaya kwa sababu watu kama Paul Pogba kukosekana kwenye michuano hiyo ni aibu, wanahitaji kucheza kwenye Ligi ya Mabingwa Ulaya ndiko viwango vyao vilipo.
“Kama watashindwa kufuzu michuanno hiyo, unaweza kuona bayana kabisa watahitaji kuondoka kwenda kwingineko. Natumai hali haitafikia huko.”