Mkwabi avuruga mambo Msimbazi

Muktasari:

Katiba ya zamani ilielekeza endapo mwenyekiti ama makamu wake akijiuzulu, basi kamati ya utendaji itamteua mtu mwenye uzoefu wa muda mrefu ndani ya klabu kuongoza kwa muda utakaobaki hadi uchaguzi utakapofanyika.

KAMA hujui leo Jumatatu umetimia mwezi mmoja kamili bila Klabu ya Simba kuwa na mwenyekiti wake, baada ya Swedi Mkwabi kujiuzulu, huku mabosi waliosalia Msimbazi wakihaha kusaka mrithi wake.
Inaelezwa mabosi wa Simba wameshindwa kumteua mtu wa kukaimu nafasi hiyo kwa vile katiba ya klabu hiyo imenyamaza, endapo mwenyekiti ama mjumbe akijiuzulu nini kifanyike tofauti na ilivyokuwa katika katiba yake ya zamani.
Katiba ya zamani ilielekeza endapo mwenyekiti ama makamu wake akijiuzulu, basi kamati ya utendaji itamteua mtu mwenye uzoefu wa muda mrefu ndani ya klabu kuongoza kwa muda utakaobaki hadi uchaguzi utakapofanyika.
Pia, katiba hiyo ilieleza uchaguzi wa kuziba nafasi hiyo unatakiwa ufanyika kwa kipindi cha miezi mitatu tangu kujiuzulu kwake ama kwao.
Lakini leo ni mwezi mzaima tangu Mkwabi alipojiuzulu nafasi ya mwenyekiti hadi sasa nafasi yake haijajazwa. Imeelezwa kutokana na katiba kutoeleza lolote juu ya kujaza nafasi hiyo hata Bodi ya Wakurugenzi ya Simba, nayo haina mamlaka ya kuteua mtu  kushika nafasi hiyo. Mwanaspoti limeambiwa ili nafasi hiyoijazwe ni lazima mkutano mkuu ufanyike.
Habari zaidi zinasema, Bodi ya Wakurugenzi itakutana muda wowote kujadili juu ya mkutano mkuu ufanyike Desemba mwaka huu.
Hata hivyo, Mwanaspoti lilimsaka a Katibu wa Simba, Dk. Anold Kashembe aliyesema maamuzi yote juu ya kujazwa kwa nafasi hiyo yatafanyika bodi itakapokutana.
“Hadi sasa hakuna mtu anayekaimu nafasi ya Mkwabi, Mkwabi alichaguliwa na wanachama, hivyo Bodi itakaa na kujadili juu ya nini kifanyike, ” alisema Dk Kashembe na kuongeza:
“Wanachama wana haki, hivyo nadhani kutakuwa na mkutano mkuu wa wanachama ndipo uchaguzi ufanyike ama itakavyoamulia.
“Ni suala la kusubiri tu muda ufike,” alisema Dk Kashembe.
Awali mara baada ya Mkwabi kujiuzulu zilikuwepo tetesi, Mjumbe wa kuteuliwa Salim Abdallah ‘Try Again’ aliyewahi kukaimu nafasi ya aliyekuwa Rais wa Simba, Evans Aveva, alikuwa akitajwa kukaimu nafasi hiyo.