Adi Yussuf, Msuva kuongoza safu ya ushambuliaji ya Tanzania

Muktasari:

Mchezo wa kirafiki kati ya Taifa Stars na Rwanda ni sehemu ya maandalizi ya mchezo wa Ijumaa dhidi ya Sudan ambao ni kwa ajili ya kuwania nafasi ya kufuzu kwa  fainali za mataifa ya Afrika kwa wachezaji wa ndani 'CHAN'

Dar es Salaam. Mshambuliaji wa Blackpool, Adi Yussuf,  Bakari Mwamnyeto wa Coastal Union na Abdul-Aziz Makame wa Yanga wameanza kwa mara ya kwanza cha timu ya taifa ya Tanzania kitakachocheza mchezo wa kirafiki dhidi ya Rwanda leo kwenye Uwanja wa Nyamirambo, Jijini Kigali.

Adi ataanza kuongoza safu ya ushambuliaji wa Taifa Stars akiwa pamoja na mshambuliaji Saimon Msuva katika kuhakikisha wanapata ushindi.

Mara ya mwisho kwa mshambuliaji Adi kupata nafasi ilikuwa chini ya Emmanuel Amunike kabla ya kutimuliwa wakati wa fainali za Mataifa ya Afrika katika mchezo dhidi ya Algeria.

Nyota huyo, aliingia kipindi cha pili, dakika ya 46 kuchukua nafasi ya Farid Mussa.

Mbali ya Adi wachezaji wengine waliopata nafasi ya kuichezea Stars kwa mara ya kwanza ni nyota wa Coastal Union, Mwamnyeto anaingia moja kwa moja kwenye kikosi cha kwanza kutokana na kusumbuliwa na majeraha kwa Kelvin Yondani.

Hivyo beki huyo wa kati, anatarajiwa kushirikiana na Erasto Nyoni kwenye safu ya ulinzi ya Taifa Stars, ambayo pia wameanza, Salum Kimenya wa Tanzania Prisons na Gadiel Michael wa Simba.

Baada ya kuonyesha kiwango bora kwenye michezo ya Ligi ya Mabingwa dhidi ya Zesco United, Makame ambaye ni kiungo mkabaji, amepewa nafasi na kaimu kocha mkuu wa Taifa Stars, Ettine Ndayiragije kuanza kwa mara ya kwanza kwenye kikosi chake.

Kikosi kamili cha Taifa Stars, Metacha Mnata, Salum Kimenya, Gadiel Michael, Bakari Mwamnyeto, Erasto Nyoni, Abdul-aziz Makame,Himid Mao, Frank Domayo, Saimon Msuva, Adi Yussuf na Farid Mussa.