Wamekalia kuti kavu ila tofauti ya Zahera, Pochettino ni hii

Muktasari:

Mashabiki wa Yanga wanaodaiwa kuwa na hasira walimbadilikia Zahera kama siye yule waliyekuwa wakimuimba na kumuona mungu mtu katika msimu uliopita, wakati Jangwani wakipiga miayo ya njaa kali.

TAYARI kuna minong’ono imeanza. Eti, Jose Mourinho anajiandaa kupata ajira yake mpya tangu alipofurushwa Man United. Anatajwa huenda akaibukia Tottenham Hotspur.
Tetesi hizi zinavumisha taarifa eti Special One ataenda kuchukua nafasi ya Mauricio Pochettino. Hizi ni tetesi zinazotolewa na vyombo vya habari.
Hata hivyo, si kazi rahisi kama inavyovumishwa. Ndio maana juzi kati, mabosi wa klabu hiyo wameweka msimamo wao, wapo nyuma ya Muargentina huyo. Kelele zote hizi zimeibuka baada ya Spurs kuwa na matokeo yasiyotabirika. Msimu huu wanaonekana kuwa ovyo.
Ni tofauti na misimu michache iliyopita na hasa wa 2016-2017 walipomaliza nafasi ya pili katika Ligi Kuu ya England.
Msimu uliopita walikuwa hatari zaidi kwani ilifika Fainali za Ligi ya Mabingwa Ulaya na kupoteza dhidi ya Liverpool, licha ya kuteleza mwishoni katika Ligi Kuu na kumaliza wa nne.
Vipigo viwili mfululizo, kimoja cha mabao 7-2 kutoka kwa Bayern Munich ya Ujerumani, kisha kucharazwa 3-0 na Brighton, huku waking’olewa na kitimu cha Daraja la Pili ya Colchester katika Kombe la Ligi, kimewavuruga baadhi ya mashabiki.
Hata hivyo hawalalamiki ama kutaka Poche atimuliwe, badala yake ni vyombo vya habari nchini humo vinatabiri kwamba huenda jamaa asiendelee kuwanoa Coys.
Utabiri huo ndio uliochangia kuanza kuibuka kwa minong’ono na kutajwa kwa Mourinho kwamba anaweza kumrithi Poche.
Hata hivyo, mashabiki wa soka wamegawanyika wapo wanaoamini kwamba Poche na vijana wake wameyumba mwanzoni wa msimu huu kwa sababu ya uchovu wa kucheza kwa nguvu misimu miwili iliyopita.
Wengine wanaamini kutajwatajwa kwake mara kadhaa kwa Poche kutakiwa Real Madrid kwenda kuchukua nafasi ya Zinedine Zidane na kabla yake pale Santiago Bernabeu, ndiko kulikomvuruga na kushindwa kufanya vyema makeke yake. Hata hivyo bado hawaonyeshi chuki yoyote na kocha huyo kwa kujua soka ndivyo lilivyo.
Hata hivyo, najaribu kuwaza tu hivi matokeo hayo yangewapata vijana wa Jangwani, chini ya Kocha Mwinyi Zahera, sijui angekuwa kwenye hali gani?
Ndio, we piga picha tu, Yanga ingepigwa mabao 7-2 pengine na Zesco United katika Ligi ya Mabingwa Afrika, kisha ikanyooshwa 3-0 na Polisi Tanzania na pengine ikalazwa na Coastal Union. Zahera angeponaje kwa wanajangwani?
Mnaweza kubisha, lakini kwa waliofuatilia pambano la Yanga katika Ligi Kuu dhidi ya Polisi Tanzania waliowatangulia mabingwa hao wa kihistoria kwa mabao 3-1 wanakumbuka kilichotokea Uwanja wa Uhuru, jijini Dar es Salaam.
Mashabiki wa Yanga wanaodaiwa kuwa na hasira walimbadilikia Zahera kama siye yule waliyekuwa wakimuimba na kumuona mungu mtu katika msimu uliopita, wakati Jangwani wakipiga miayo ya njaa kali.
Maneno ya ovyo na yenye karaha toka kwenye vichwa vya mashabiki wa Yanga waliokuwa jirani na Zahera jukwaani kwenye mchezo huo, vilimfanya kocha huyu asiwe na hamu ya kurejea tena eneo hilo baada ya mapumziko.
Bila shaka alihoia usalama wake na pia hakupenda kusikia kejeli alizokuwa akipewa. Mashabiki hao walimsapraizi, kwani hakuwahi kusikia akipondwa kama alivyopondwa siku hiyo.
Bahati nzuri mechi iliisha kwa sare ya 3-3 baada ya David Molinga kufunga mara mbili, ambapo baadhi ya waliokuwa wakimtusi Zahera na kutaka atimke zake ili aawachie timu yao, walisahau na kushangilia matokeo na kumuimba Molinga!
Wapo walioendelea kumsimanga na kutaka atimuliwe kikosini, lakini kuna wale ambao nyuso zao zimeumbwa na haya na kubaini Zahera bado anahitajika mno ndani ya Yanga kwa sababu ya mambo yanayoendelea.
Bahati mbaya mashabiki wa soka ni watu wasiotabirika. Dakika moja wanakuimba, dakika nyingine wanakutukana! Ni vigeugeu kwelikweli kuliko hata Kinyonga.
Mashabiki wanamlalamikia Zahera kwamba amefanya usajili wa ovyo msimu huu, wakati aliachiwa kila kitu akifanye baada ya msimu uliopita kukuta timu kushindwa  kumpa mahitaji yake kwa vile haikuwa na fedha.
Lakini mashabiki hao wanasahau, Yanga ya sasa ni mpya. Inaundwa na asilimia kubwa ya wachezaji wapya ambao hawajaunganisha na kuzoeana kuipa timu matokeo.
Ukiacha timu kukosa muunganiko kwa vile bado ni mpya, lakini pia kuna suala la majeruhi na madeni ya wachezaji ambao yanakivuruga kikosi, tofauti na mashabiki wanaiangalia timu yao.
Inawezekana ni kweli Zahera amechemsha katika kufanya usajili, lakini bado sioni kama ni wakati muafaka wa kocha huyo kuonyeshwa mlango wa kutokea kama  mashabiki wenye jazba wanavyoshinikiza kwa viongozi wa klabu hiyo.
Bahati mbaya ni kwamba viongozi wa Yanga wala hawajitokezi kuonyesha msimamo wao. Hawaonyeshi kama wanamuunga mkono kocha wao na kuwanyamazisha mashabiki kwa kuhofia nao kubadilikiwa. Hii ndio tofauti ya wao na sisi katika soka.
Kadhalika timu kufungwa ama kutoka sare au kushinda ni sehemu ya mchezo. Spurs kapasuka 7-2 na kisha kupigwa 3-0, lakini huwezi kusikia mashabiki wa Coys wakitaka kocha atimuliwe kwa sababu wanafahamu kuna utamu na uchungu kwenye soka.
Kama walivyokuwa wakipata utamu Spurs ikipata matokeo kwenye michuano ya msimu uliopita, hata sasa wanapopata uchungu wanajua ni sehemu ya mchezo na wanaamini timu yao itakaa vizuri hata kama Poche amejizingua mwenyewe kwa kuwazuia wachezaji waliokuwa wanataka kuondoka kikosini.
Yanga imefungwa bao 1-0 na Ruvu Shooting na kutoka sare ya 3-3 na Polisi kisha kushinda 1-0 dhidi ya Coastal, matokeo ambayo sio ya kukatisha tamaa au ya kufanya Zahera aonekane hafai kwa sasa, labda tu kama hawamhitaji tu kwa suala jingine.
Lakini Wanayanga wanapaswa kutambua kwa sasa, timu yao ina kibarua kizito mbele ya Pyramids FC ya Misri katika mechi za playoff kuwania Kombe la Shirikisho Afrika.
Kadhalika Yanga ni kama timu nyingine ambazo nazo zinashinda na kufungwa. Kama Barcelona na Lionel Messi wao wanafungwa au kupata sare, Yanga ni timu gani isionje matokeo ya hivyo. Iwapo watetezi wa Ligi Kuu England, Man City inalala mbele ya wapinzani wao kwenye ligi hiyo licha ya kuwa na kikosi bora na kocha mwenye rekodi zake, Pep Guardiola, Yanga ya Zahera ni timu gani hata isiweze kuambulia japo sare? Utamaduni huu wa mashabiki kutotaka kuona timu zao zikifungwa haupo Yanga tu! Hata Simba na klabu nyingine wana kasumba hiyo. Hawachelewui kuwageuka makocha wao na kuwaona hawafai kwa sababu ya matokeo ya mechi moja ama mbili. Nani amesahau kama mashabiki wa Msimbazi wa jijini Mwanza walimpopoa chupa tupu za maji, Kocha Patrick Aussems kwa vile tu, Simba ilitoka suluhu Ndanda kabla ya kula kichapo cha 1-0 kutoka kwa Mbao kwenye Uwanja wa CCM Kirumba.
Hata hivyo, mwishowe, si hao hao waliomshangilia tena kocha huyo wakati timu ikichukua ubingwa kabla Ligi haijamalizika na kurejea tena msimu uliopita, kuonyesha kuwa mashabiki wa soka ni vigeugeu na wasio na subira kwa timu zao.
Lakini ifike wakati mashabiki na hata wanachama wa klabu za soka nchini kubadilika na kuishi katika dunia ya usasa, waache kukariri na kuamini timu zao hazifungiki wala kupata matokeo mabaya.
Hiyo itasaidia angalau kupunguza tofauti ya soka letu na lile la wenzetu ambao, wanaamini soka ni mchezo wa makosa na lolote hutokea!