Yanga kujifua kwa Friends Rangers, Pan African kuikabili Pyramids FC

Thursday October 10 2019

Mwanaspoti, Yanga kujifua kwa, Friends Rangers, Pan African kuikabili, Pyramids FC, Tanzania, Kombe la Shirikisho Afrika

 

By Yohana Challe

Dar es Salaam. Baada ya kupangwa kucheza na Pyramids FC ya Misri katika hatu ya mtoano ya Kombe la Shirikisho Afrika, uongozi wa Yanga umeanza mikakati ya kuhakikisha inapata ushindi mnono katika mchezo wa kwanza utakaofanyika jijini Dar es Salaam. 

Yanga itaanzia nyumbani Oktoba 27 kwenye Uwanja wa Taifa kabla ya kurudiana ugenini Novemba 3 na mshindi wa jumla wa mchezo huo atatinga moja kwa moja hatua ya makundi.

Ili kujipanga na mchezo huo, Yanga itacheza michezo miwili ya kirafiki dhidi ya timu za Ligi Daraja la Kwanza Friends Rangers Oktoba 12 kisha kuivaa Pan African Oktoba 16.

Mhamasishaji wa timu hiyo, Antonio Nugaz aliwataka  mashabiki na wanachama wa klabu hiyo kuacha kutishika na rekodi za wachezaji  Pyramids ambao wamenunuliwa kwa bei kubwa, huku akiwaomba kushikamana ili kushinda mchezo wa nyumbani.

"Hatudharau wala hatuchukulii poa na hatutishwi na uwekezaji wao kwa sababu mpira unachezwa uwanjani, hivyo tumefurahi kupangwa nao kwasababu janjajanja zao tunazijua kwa muda mrefu na hakuna hofu.

"Licha ya timu yetu kuanza msimu kwa kusuasua, lakini sasa iko vizuri hivyo tutahakikisha tunawashawishi wadhamini wetu kufanya liwezekanalo ili kuwapa motisha wachezaji, ili waweze kufanya vizuri katika mchezo huo" alisema Nugaz.

Advertisement

Advertisement