DC Motema Pembe, Paradou, Pyramids FC tishio kwa Yanga Kombe la Shirikisho

Muktasari:

Katika kundi hilo la timu 10 ni timu tatu tu ambazo zinaonekana kuwa tishio kwa Yanga ambazo ni DC Motema Pembe, Paradou na Pyramids FC.

Dar es Salaam. Leo Jumatano saa 2:00 usiku Yanga itajua ni timu ipi kati 10 itapangwa nayo katika mechi ya mtoano ya kusaka kufuzu kucheza hatua ya Makundi ya Kombe la Shirikisho.

Katika kundi hilo la timu 10 ni timu tatu tu zinaonekana kuwa tishio zaidi kwa Yanga ambazo ni DC Motema Pembe (DR Congo), Paradou (Algeria), Pyramids FC (Misri).

Mechi ya kwanza ya hatua ya mtoano itaanza kuchezwa Oktoba 27, 2019 wakati mechi ya marudiano itakuwa Novemba 3, 2019.

Kwa mujibu wa CAF, Yanga imepangwa Chungu A hivyo itacheza na moja ya timu kutoka Chungu D ambazo nyingi siyo timu tishio katika mashindano ya klabu barani Afrika.

Mwanaspoti Online inakulete rekodi ya wapinzani kumi 10 wa Yanga jinsi walivyopita hadi kufikia hatua hiyo ya kupigania nafasi ya kuingia makundi ya kombe la Shirikisho Afrika.

DC Motema Pembe (DR Congo)

Imefanikiwa kufika hapo baada ya kuitoa Al Khartoum ya Sudan kwa penalti 3-1 baada ya mchezo wa kwanza Motema kushinda 2-1 na mchezo wa marudiano kufungwa 2-1 na kutupika penalti kumpata mshindi huyo.

Nyota wao ni mshambuliaji Serge Lofo anayecheza timu ya taifa ya DR Congo, pia wapo waliowahi kupita Tanzania, Nkanu Mbiyavanga na Lino Masombo walicheza Simba.

Bandari FC (Kenya)

Chini ya kocha Ben Mwalala aliyewahi kuwika akiwa mshambuliaji wa Yanga, wamefanikiwa kufikia hatua baada ya kufanya vizuri tangu hatua za awali.

Bandari ilifanikiwa kuitoa Al Ahli Shandi kwa kuifunga kwa sheria ya bao la ugenini baada mechi yakwanza kutoka suluhu Mombasa na waliporudiana Sudan wakatoka sare 1-1.

Pia, Bandari ilitoa Ben Guerdane baada ya mchezo wa kwanza nyumbani mabao 2-0 na mechi ya marudiano walifungwa 2-1 Tunisia.

Triangle United (Zimbabwe)

Waliiondoa Azam ya Tanzania kwenye raundi iliyopita kwa matokeo ya jumla ya mabao 2-0, moja ya siri ya mafanikio kwa timu hiyo ni mbinu za kocha wao, Taurai Mangwilo ambaye aliibana Azam wakiwa Chamazi kiasi cha kushindwa kupenya kwenye ngome yao.

Bidvest Wits (Afrika Kusini)

Moja ya wachezaji hatari kwenye kikosi hicho, ambacho kinafundishwa na Gavin Hunt ni Mxolisi Macuphu ambaye kwenye michezo sita ya Ligi Kuu Afrika Kusini, ameifungia timu hiyo, mabao matatu licha ya kuwa ni kiungo.

TS Galaxy (Afrika Kusini)

Katika hatua iliyopita ya kombe la shirikisho, aliyekuwa shujaa kwenye kikosi hicho ni Barns Sanele mwenye miaka 22, kiungo huyo aliifungia timu hiyo mabao matatu kwenye jumla ya matokeo ya mabao 4-2, ambayo waliyapata dhidi ya CNaPS Sport.

ESAE FC (Benin)

Antonin Oussou na Emmanuel Onyenwen ni wachezaji ambao wamekuwa na mchango mkubwa kwa timu hiyo, kufika katika hatua ya mchujo licha ya kuwa katika raundi iliyopita walivuka kwa matuta baada ya kutoka suluhu kwenye michezo yote miwili, nyumbani na ugenini.

FC San Pedro (Ivory Coast)

Licha ya kutokuwa na wastani mzuri wa kufunga, Christ Mbondi amekuwa akitegemewa kwenye kikosi cha FC San Pedro, nyota huyo raia wa Cameroon aliwahi kuwika akiwa na Rayon Sports ya Rwanda.

Paradou (Algeria)

Kama Yanga watapangwa na timu hii ya Algeria, watakumbana na mbinu za kocha wa Kireno, Francisco Chaló. Hakuna mshambuliaji mwenye hata mabao mawili kwenye kikosi cha timu hiyo ndani ya michezo mitano ya Ligi.

Pyramids FC (Misri)

Ni miongoni mwa timu ambazo zimeuanza vizuri msimu huu wa Ligi Kuu Misri chini ya kocha wao, Mfaransa Sébastien Desabre waliing’oa Belouizdad kwenye raundi ya kwanza kwa ushindi wa jumla ya mabao 2-1.

Proline (Uganda)

Hii inaweza kuwa timu nyepesi zaidi kwenye chungu D ambapo moja ya timu za kundi hilo, zitapangwa na Yanga, Proline wapo kwenye hatari ya kushuka daraja licha ya kutinga hatua ya mchujo kwa kuwaondoa AS Kigali kwa ushindi wa jumla ya mabao 3-2.