Samatta Mtanzania wa kwanza kuwa nahodha Ligi ya Mabingwa

Muktasari:

Kwa mara ya kwanza kwa Samatta kuvaa kitambaa hicho ilikuwa ni kwenye mchezo wa Ligi Kuu Ubelgiji dhidi ya Oostende, Septemba 21.

Dar es Salaam. Mshambuliaji wa Kimataifa wa Tanzania, Mbwana Samatta anatarajiwa kuweka rekodi ya kuiongoza klabu yake ya KRC Genk kwa mara ya kwanza akiwa nahodha katika mchezo wa Ligi ya Mabingwa Ulaya dhidi ya Napoli.

Kutoanza kwa Sébastien Dewaest katika kikosi cha kwanza cha timu hiyo kumetoa nafasi kwa Samatta kuweka rekodi katika mchezo huo wa kwanza kwa KRC Genk kucheza nyumbani.

Samatta ambaye pia ni nahodha wa timu ya Taifa ya Tanzania, 'Taifa Stars' anakuwa mchezaji wa kwanza wa Kitanzania kuvaa kitambaa cha unahodha katika mchezo wa Ligi ya Mabingwa Ulaya.

Katika mchezo wa kwanza wa hatua hii ya makundi ambao KRC Genk walicheza dhidi ya Salzburg na kupoteza kwa mabao 6-2, Samatta aliweka rekodi ya kuwa Mtanzania wa kwanza kucheza mashindano hayo.

Licha ya kupoteza katika mchezo huo wakiwa ugenini, aliweka rekodi ya kuwa mchezaji wa kwanza kutoka ukanda wa Afrika Mashariki kufunga bao katika mchezo wake wa kwanza wa Ligi ya Mabingwa.

Wapinzani wa KRC Genk katika mchezo wa leo, Napoli waliifunga Liverpool nchini Italia kwa mabao 2-0 hivyo Samatta anakibarua kizito kuhakikisha wanafanya vizuri katika mchezo huo.