Yanga yatua Dar, Zahera akili yote kwa Polisi Tanzania

Muktasari:

Zahera ametoa kauli hiyo muda mfupi baada ya timu ya Yanga kuwasili Dar es Salam leo usiku huu ikitokea Zambia ilipokwenda kucheza mchezo wa marudiano wa Ligi ya Mabingwa Afrika dhidi ya Zesco na kung'olewa kwa jumla ya mabao 3-2.

Dar es Salaam. Kocha wa Yanga, Mwinyi Zahera amesema akili yake sasa ni katika mchezo ujao wa Ligi Kuu Tanzania Bara dhidi ya Polisi Tanzania.

Zahera ametoa kauli hiyo muda mfupi baada ya timu ya Yanga kuwasili Dar es Salam leo usiku huu ikitokea Zambia ilipokwenda kucheza mchezo wa marudiano wa Ligi ya Mabingwa Afrika dhidi ya Zesco na kung'olewa kwa jumla ya mabao 3-2.

Baada ya kuwasili Uwanja wa Ndege, wachezaji wa Yanga hawakutaka kuongea lolote kwani walionekana kuwa na hasira wakielekea lilipoegeshwa gari la kuwa chukua.

Kocha Zahera alisema kilichotokea katika mchezo huo, sio jambo la ajabu katika soka na sasa wamerejea ili kujipanga na michezo iliyokuwa mbele yao.

"Hakuna wa kumlaumu, kilichotokea ni sehemu ya mchezo, kuhusu tatizo la ufungaji nimelizungumza mara nyingi hivyo sihitaji kulirudia tena.

"Tulipanga kupata bao la mapema katika mchezo, lakini wao wakapata nasi tulifunga, hivyo matokeo hayakuwa mazuri kwa kila mmoja upande wetu ndio maana anasema kila kitu kimepita na sasa tunajipanga na mengine," alisema Zahera.