Fei Toto: Zesco watapigwa kwao bila shaka

Muktasari:

Yanga haina presha katika mechi yao ya marudiano na Zesco, mechi ya Ligi ya Mabingwa Afrika, nyota wa timu hiyo Fei Toto anaamini wanashinda.

Dar es Salaam. Kiungo Feisal Salum ‘Fei Toto’ amewahakikishia ushindi mashabiki wa Yanga katika mchezo wao wa Jumamosi dhidi ya Zesco ya Zambia.

Yanga inakwenda katika mchezo huo ikiwa kumbukumbu ya kulazimishwa sare 1-1 nyumbani na Zesco hivyo wanahitaji ushindi au sare ya kuanzia mabao mawili ili kufuzu kwa hatua ya makundi ya Ligi ya Mabingwa.

Akizungumzia mchezo huo Fei Toto alisema mashabiki wanatakiwa kuwaamini wachezaji na kuitakia mema timu katika mchezo huo ili waweze kusonga mbele.

"Zesco walikuja kucheza Tanzania kwa kusaka matokeo kwani sisi tutashindwa nini kusaka matokeo kwenye mechi ya marudiano kwao."

"Ni kweli utakuwa mchezo mgumu ila wao ndio watakuwa na presha ya hali ya juu kwani watakuwa wanataka kuwaonyesha mashabiki wao kwamba wanafanya vyema."

"Kwa upande wetu ni kama tupo vitani kuiwakilisha nchini yetu kwa ushindi, hivyo tutaingia uwanjani kwa nguvu zetu zote, ushindi ni lazima hata kama wapinzani wetu ni wazuri kiasi gani,"alisema Fei Toto.

Yanga ilitoka sare ya bao 1-1 na Zesco mechi iliopigwa Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam, Jumamosi ya wiki hii wanatarajia kushuka dimbani ugenini.