Aussems ataka ushindi tu kwa Kagera Sugar

Muktasari:

Simba imewasili kwenye uwanja wa Ndege mjini Bukoba leo tayari kwa mchezo wao wa kesho wa Ligi Kuu dhidi ya Kagera Sugar wakiwa na kumbukumbu ya kufungwa mabao 2-1 msimu uliopita kwenye Uwanja wa Kaitaba.

Dar es Salaam. Kocha wa Simba, Patrick Aussems amesema kikosi chake kimefika salama Kagera na wachezaji wanamorali ya kuvunja rekodi mbaya dhidi ya Kagera Sugar.

Simba imewasili Kagera leo asubuhi tayari kwa mchezo wake wa kesho Alhamisi dhidi ya wenyeji wao Kagera Sugar kwenye Uwanja wa Kaitaba.

Mbelgiji anatua Kagera akiwa na kumbukumbu ya kupoteza mechi mbili za msimu uliopita dhidi ya wenyeji wake hao.

"Tutafanya mazoezi mepesi na kuzoea uwanja jioni ya leo, lakini kwetu maandalizi yote tulimaliza tukiwa Dar es Salaam, jambo ambalo linatupa morali ya kuja kuvunja rekodi mbaya dhidi ya Kagera na maandalizi yetu ambayo tumefanya naimani linawezekana hilo," alisema Aussems.

Haruna Shamte alisema wanataka kufuta rekodi yao mbaya kwa Kagera Sugar.

Shamte alisema mpinzani wao anapojiamini kupitiliza kwao ni faida kujituma na kupata matokeo akisisitiza kwamba licha ya kuheshimu uwezo wa Kagera Sugar hautawazuia malengo yao.

"Timu ambazo zinakaa na wachezaji kwa muda mrefu ni nzuri kwani wanakuwa wanajuana kama ilivyokuwa kwa Kagera Sugar, lakini kwa sasa kikosi chao kimebadilika."

"Tunajua siyo mechi ya kupata mtelemko ndio maana tumefanya mazoezi ya nguvu kuhakikisha tunakuwa fiti kwa ajili ya mchezo huo, mechi itakuwa ngumu ila tutapambana," alisema Shamte.

Naye kiungo Jonas Mkude alisema kwa ufupi mechi hiyo kwamba dakika 90 ndio mwamuzi wa mchezo huo na kwamba ya msimu uliopita hayana nafasi kwao.

"Mchezaji yoyote anapocheza akili yake unakuwa inawaza ushindi tunaangalia mechi ya kesho na sio nini kilitokea msimu ulioisha hapo tutakuwa hatufiki kwenye malengo yetu"alisema.

Wakati mastaa wa Simba wanawaza kuvunja mwiko kwa upande wa beki wa Kagera Sugar, David Luhende alisema mchezo wa kesho utawashangaza wengi.

"Simba wanafungwa kwa sababu saikolojia zao zinakuwa zinatuwazia tofauti hilo halitufanyi tuone mchezo rahisi, Kuna wachezaji wapo vizuri kiufundi ila tutapambana nao," alisema Luhende.