Hii kasi ya Allan Wanga, kiatu lazima

Muktasari:

Wanga kashika usukani kwenye jedwali la mabao mpaka sasa akimpiku mshindani wake wa karibu sana msimu uliopita Enos Ochieng (Ulinzi Stars), aliyepachika mawili sawia na nahodha wa Gor mahia kiungo mbunifu Kenneth Muguna na Kepha Namanya (Zoo)

STRAIKA mkongwe Allan Wanga kaanza kuifukuzia tena kiatu cha dhahabu, akiwa tayari ni kinara wa mabao baada ya mzunguko wa tatu wa Ligi Kuu ya KPL msimu huu.
Wanga aliyetangaza kustaafu soka la kimataifa miezi miwili iliyopita, akiwa na umri wa miaka 34, tayari ashapachika mabao matatu baada ya kumaliza msimu uliopita akiwa mfungaji bora kwa kutia kimyani 17.
Juzi Jumapili Kakamega Homeboyz ilipoikaribisha nyumbani Kariobangi Sharks uwanjani Bukhungu, na kuvuna ushindi mnene wa magoli matatu kwa mtungi, Wanga alipachika mawili.
Nahodha huyo alitia kimyani bao lake la pili kwenye msimu na vile vile la pili kwenye mechi hiyo kunako dakika ya 52 baada ya kumalizia krosi ya frikiki kutoka kwake Festus Okiring.
Goli la tatu la mchezo huo na pia lake la tatu kwa ujumla baada ya mizunguko mitatu ligini, alilipachika kunako dakika ya 67 kupitia mkwaju wa penalti.
Kwa idadi hiyo, Wanga kashika usukani kwenye jedwali la mabao mpaka sasa akimpiku mshindani wake wa karibu sana msimu uliopita Enos Ochieng (Ulinzi Stars), aliyepachika mawili sawia na nahodha wa Gor mahia kiungo mbunifu Kenneth Muguna na Kepha Namanya (Zoo)
Msimu uliopita ushindani wa kiatu cha dhahabu uliokuwa baina ya wawili hao kuelekea mwisho wa msimu, ulizua utata baada ya Ochieng kumfunika Wanga kwa kupachika mabao 20.
Hata hivyo katika hali isiyo ya kawaida Ochieng alivuliwa taji hilo la mfungaji bora wa msimu uliopita na ikakabidhiwa Wanga licha ya kupachika mabao 17.
Utata huo ulikuwa kama hivi. Msimu uliopita 2017/18 kwenye raundi ya mwisho wa msimu wa ligi kuu, Ulinzi Stars waliwalima Mt Kenya mabao 4-0. Mechi hii ilikuwa ni marudio baada ya kutibuka hapo awali pale wachezaji wa Mt Kenya walipogoma kucheza kwenye siku iliyoratibiwa ili kulalamikia kutolipwa mishahara yao.
Timu zote ligini zilikuwa zishamaliza mechi zao ikawa imesalia hiyo iliyoamrishwa na KPL irudiwe baada ya kutibuka.
Mpaka hapo wafungaji bora walikuwa ni Enos  na Wanga kila mmoja akiwa na mabao 17.
Kutokana na maagizo hayo ya KPL, Ulinzi waliishia kuwalima Mt Kenya  mabao manne, huku Ochieng akifunga matatu kwenye mechi hiyo na hivyo kumwezesha kumaliza na jumla ya mabao 20.
Marudio ya mchuano huo ukaipelekea Homeboyz kuandikia barua  Kamati ya kinidhamu ya ligi kuu IDCC ikilalamikia  marudio ya mechi hiyo kwa kusisitiza  haikumtendea haki straika wao Wanga kwenye  harakati za kusaka kiatu cha dhahabu.
Kakamega walihoji kwamba kimsingi timu inaposusia mechi kwa mujibu wa ratiba, basi mpinzani wake huzawadiwa ushindi wa mabao matatu na ndivyo ilivyostahili kufanyika na wala sio mechi kurudiwa kwani waliosusa ndio waliokosea.
Kwenye maamuzi yake IDCC ilikubaliana na mawazo ya Kakamega. Iliishtumu Mt Kenya kwa kususia mechi hiyo kimakusudi na hivyo kusema hapakuwa na haja ya kurudiwa.
Kutokana na hilo ikafutilia mbali matokeo ya marudio ya mechi hiyo ya ushindi wa Ulinzi wa mabao 4-0. Badala yake ilizawadiwa Ulinzi na ushindi na mabao matatu. Kwa maana hiyo yale matatu aliyopachika Enosh kwenye ushindi huo yakafutwa na hivyo kumweka sawa kwenye idadi ya mabao ya wafungaji bora msimu huo kuwa sawa na za Wanga 17.