Aussems atafuta dawa ya Simba kulipa kisasi kwa Kagera Sugar

Muktasari:

Katika mazoezi hayo Aussems alipanga vikosi viwili na kucheza mfumo wa 3-5-2 na muda mwingine alikiwa akichanganya na kucheza 4-4-2.

Dar es Salaam.Kocha wa Simba, Patrick Aussems ametafuta dawa ya kulipa kisasi kwa Kagera Sugar baada ya kucheza mfumo wa 3-5-2 na muda mwingine alikiwa akichanganya na kucheza 4-4-2 katika mazoezi ya leo kwenye Uwanja wa Gymkhana, Dar es Salaam.

Simba msimu uliopita ilipoteza michezo yote miwili dhidi ya Kagera Sugar baada ya kufungwa 1-0 (Uhuru) na 2-1 (Kaitaba).

Akizungumzia mchezo wao dhidi ya Kagera Sugar, Mbelgiji huyo alisema timu hiyo imekuwa ikiwasumbua mara kwa mara, lakini safari hii wanataka kuhakikisha wanatoka na ushindi.

"Kagera wamekuwa wakitusumbua katika msimu uliopita, safari hii tumefanya mazoezi kwa umakini mkubwa kuhakikisha tunafanya kitu cha tofauti," alisema Aussems.

Aussems aligawa wachezaji Aishi Manula, Pascal Wawa, Tarone Santos, Shomari Kapombe, Mohamed Hussein 'Tshabalala', Mzamiru Yassin, Francis Kahata, Sharaf Shiboub, Hassan Dilunga na Meddie Kagere katika kikosi kilichokuwa kimevaa Bips.

Huku katika kikosi cha pili kikiwa Beno Kakolanya, Kennedy Juma, Yusuph Mlipili, Haruna Shamte, Gadiel Michael, Said Ndemla, Jonas Mkude, Miraj Athuman, Deo Kanda, Ibrahim Ajib na Wilker Da Silva.

Baada ya kucheza takribani dakika 15, Aussems alibadilisha baadhi ya wachezaji baada ya Mkude kuvaa bips na kwenda kuchukua nafasi ya Dilunga, Gadiel alitoka na kwenda kufanyiwa masaji na nafasi yake ilichukuliwa na Rashid Juma ambaye alikuwa yupo nje ya uwanja akifanya mazoezi ya viungo, wakati huo huo Kahata alivua bips na nafasi yake ilichukuliwa na Wilker Da Silva ambaye alienda kucheza na Kagere.

Simba inatarajia kucheza na Kagera Sugar Septemba 26, huku wao wakiondoka kwa usafiri wa ndege kesho asubuhi Septemba 25.