Dilunga, Mo Banka wanukia zao Ulaya

KWENYE sehemu ya kwanza ya makala haya jana Alhamisi tulifahamu kuhusu wakala Mtanzania Zuberi Kambi na Mcameroon Alex Morfaw waliohusika kuwapeleka kucheza soka Marekani nyota wa Kitanzania, Abdallah Shaibu ‘Ninja’ na Ally Ng’anzi. Endelea…

DILUNGA ANUKIA ULAYA

Wakati Ninja na Ng’anzi wakiendelea kutengeneza njia yao huko Marekani, neema imeanza kung’ara kwa kiungo wa Simba, Hassan Dilunga ‘HD’.

Uwezo unaoonyeshwa na kiungo huyo wa zamani wa Yanga pale Msimbazi ni mkubwa sana kiasi cha kurejeshwa timu ya Taifa.

Wakati stori mbili-tatu na Mwanaspoti zikiendelea huku Alex akiwa, pembeni Kambi alimuuliza Alex kuhusu Dilunga na jamaa anajibu bado anashangaa kuona mchezaji huyo akicheza Bongo.

“Dilunga hivi sasa yupo katika kiwango kizuri na jamaa amevutiwa naye kweli kweli, kikubwa tuombe aendelee kuonyesha hivi hivi,” anasema.

Anaongeza uwepesi wa Dilunga kuondoka utawezekana mwishoni mwa msimu kwani mkataba wake utakuwa umemalizika. Wakati huohuo, kwa upande wa wachezaji wake Kelvin Nashon na Issa Makamba wao wataondoka nchini muda wowote kuanzia sasa kwenda kucheza soka la kulipwa nje ya nchi.

“Nashon ataenda katika kituo ch vipaji Canada, Issa yeye kapata timu Israel, tunataka kufanya kama sehemu ya kuanzia kwanza ili baadaye waweze kupata sehemu nzuri zaidi,” anasema Kambi.

AFICHUA SIRI ZA DILUNGA

Kambi anasema alikaa na Dilunga na kuzungumza naye changamoto alizopitia baada ya mambo ya soka kuwa mengi.

“Unajua Hassan alipoenda Yanga alikuwa mdogo sana kwa hiyo alipotoka alihisi kama hatoweza kurejea katika kiwango chake na ndipo tatizo lilianzia hapo,” anasema.

Anaongeza alipokutana naye wakati anasaini Mtibwa Sugar alimwaminisha hajapotea na kweli aliweza kufanya vizuri na kila mmoja alivutiwa na kiwango chake.

“Nashukuru Mungu Dilunga aliweza kurejea katika hali yake ya kawaida na kujituma uwanjani kitu ambacho nilikuwa nataka kukiona kutoka kwake, mpaka anaenda Simba ndio nilikuwa nahitaji iwe hivyo.”

KESI YA MO’ ISSA BANKA

Kiungo Mohammed Issa ‘Banka’ mwanzoni mwa msimu uliopita alijikuta akifungiwa kucheza soka baada ya kubainika kutumia dawa zinazopigwa marufuku michezoni.

Wakati huo Banka alikuwa yupo katika kiwango cha juu na msimu 2018/19 ndio ulikuwa unakaribia kuanza lakini tetesi za kufungiwa zilianza kutibua mipango ya usajili kucheza katika timu kubwa nchini.

Kambi anafichua Banka alikuwa akihitajika Azam, Simba na Yanga lakini kesi yake ilitaka kutibua usajili kabla ya Yanga kumalizana naye.

“Dah, nakumbuka ilikuwa ngumu mno ile kesi, timu tatu zilikuwa zikimhitaji kwa nia ya kweli kabisa, lakini tetesi zilipoanza zilitaka kuharibu. Nashukuru jambo lile lilipita na hivi sasa anaitumikia timu yake kwa hali ya juu,” anasema.

Anaongeza Banka alikata tamaa, lakini alijitahidi kumweka katika hali nzuri ya kujiona bado ana uwezo wa kufanya kitu katika mpira.

“Nawashukuru Yanga kwa kumvumilia kwa sababu ilikuwa miezi yupo nje ya uwanja, kwa hiyo acha amalizie msimu wake wa mwisho tuone itakuaje.”

ANANUFAIKAJE?

Kila kazi ina malipo yake. Kwa upande wa Kambi anaweka wazi kwa usajili wa ndani amekuwa hachukui pesa yoyote kwa wachezaji wake kwani lengo lake ni kuona wanafanikiwa kufika mbali.

“Hawa wote ambao wapo wanacheza soka la hapa wala sijawahi kuchukua pesa yao, labda wao wenyewe wanipe kama ahsante na hiyo hadi kwenye mikataba yangu nimeandika kabisa sichukui pesa ya usajili wa ndani,” anasema.

Anaongeza kwa usajili wa nje ambao ndio wenye pesa nyingi ndio anatolea macho na hiyo ndio sababu kubwa ya kujikita zaidi kuhakikisha wachezaji wanaenda nje.

“Nipo katika kusaidia zaidi, hawa waliotoka nje nao bado sijaonja, lakini pesa ipo kwani wapo sehemu nzuri ambayo naamini kabisa wataonekana kwenda klabu nyingine.”

KUMBE ANATAMBULIKA

Licha ya kufahamika kwa umeneja, Kambi pia hivi sasa ni wakala wa FIFA, baada ya kuwa na leseni yake mkononi.

Kuhusu kumudu kazi zote mbili kwa mpigo, alifunguka ana kituo chake cha Cambiasso Sports Managament, hivyo kuna watu ambao anasaidiana nao kuhakikisha kila kitu kinaenda sawa.

“Unajua hizi kazi ni kushirikiana na watu ambao naamini nao wana jicho la kuona kitu, kwahiyo tuna kituo chetu na ndio wanashughulika kuangalia wachezaji,” anasema.

Anaongeza jambo zuri hivi sasa tayari amepata leseni ya uwakala ambayo itakuwa inamfanya azungumze na klabu yeye mwenyewe.

‘MZUNGU’ ANAVYOUNGANISHWA

Muda wote ambao nilikuwa napiga stori na Kambi, pembeni alikuwepo Mcameroon Alex Morfaw ambaye alikuwa bize na laptop yake (kompyuta mpakato) akionekana kuandika baadhi ya vitu.

Nilimwita kwa jina lake aligeuka na kunionyeshea tabasamu ndipo nikaanza kuzungumza naye na kuweka wazi namna ambavyo anafanya kazi na Kambi kuhakikisha kila kitu kinakuwa sawa kwa wachezaji hao kupata soko Ulaya.

Alex anaweka wazi alibahatika kuangalia mechi moja ya vijana ndipo akamwona Ally Ng’anzi na kuvutiwa nae, ndipo akaanza kulitolea macho soka la Bongo.

“Baada ya kuja Tanzania kukutana na Kambi ilibidi nionane na mchezaji mwenzangu wa zamani Vancouver, Nizar Khalfan na ndipo nikawa nachukulia Tanzania kama nyumbani kwa sababu tayari nilikuwa na wenyeji wangu wawili,” anasema.

“Niliishi vizuri na Nizar kule Marekani, walikuwa wanakuja kunitembelea nyumbani kwangu na hata muda mwingine tulikuwa tukitoka na mimi nilikuwa dereva wao mara kwa mara,” anasema.

Wakala huyo alisema kutokana na kuwa na wenyeji wawili nchini ilimfanya kujihisi yupo nyumbani na kuzidisha safari za kuja mara kwa mara na ndipo alipobahatika kumwona Abdallah Shaibu ‘Ninja’.

“Nilimwambia Kambi namhitaji Ninja basi kweli kabla ligi haijaisha tulizungumza naye na tukamwambia asisaini mkataba wowote mpya, ikawa hivyo mpaka anasaini mkataba wa kwenda MFK Vyskov na kutolewa kwa mkopo kwenda LA Galaxy inayoshiriki Ligi Kuu ya Marekani.”

MCHONGO MZIMA UPO HIVI

Maswali yalikuwa mengi namna ambavyo wachezaji Ally Ng’anzi na Ninja kusaini Czech na kisha kutimkia zao Marekani, hiyo inashtua kutokana na nchi yetu ilivyo.

Nikiwa bado nipo na Alex nilimwona akiweka laptop yake pembeni kisha akaniambia anajua hilo jambo lazima litakuwa na maswali mengi.

Alex anasema ukaribu wake na klabu za Marekani ndio umechangia yeye kuwa mwepesi kuhakikisha wachezaji wanaingia Marekani kwa sababu tayari ameaminika.

“Unajua mimi nilikuwa nacheza mpira zamani lakini majeraha ndio yamenifanya niachane na soka, ni rahisi sana Thomas rafiki yangu kwa sababu niliishi vizuri na timu ndio maana naaminika hivi sasa,” anasema.

Alion geza: “Sio tu upande wa Marekani bali hata upande wa Ujerumani na Uingereza nako nina watu wangu, lakini ni ngumu kumtoa mchezaji hapa na kwenda moja kwa moja Uingereza.”

NINJA, NG’ANZI TAA YA KIJANI

Alex anafichua kabisa soka letu lipo chini tofauti na Marekani, lakini uwepo wa wachezaji hao katika Ligi Kuu kutatoa mwanga mzuri kuelekea katika maisha yao ya soka.

“Ninja leo yupo timu moja na Zlatan Abrahimovic, unadhani baada ya muda kidogo atakuwa yule ambaye ametoka Yanga? Sikatai ana uzoefu wa kutosha lakini kule anaongezeka na ataongezeka vitu vingi,” anasema.

Wakala huyo anaongeza hata kwa upande wa kiungo Ally Ng’anzi ni rahisi hivi sasa kucheza katika ligi kubwa zaidi kutokana na tayari amepata uzoefu wa kutosha.

“Ally tayari ameshacheza na Aston Villa mchezo wa kirafiki, kupewa tu dakika katika mchezo ule ni jambo kubwa kwahiyo ni rahisi kwenda sehemu yoyote hivi sasa kikubwa ni kuendelea kwake kujituma na vitu vingine vinawezekana kabisa,” anasema.

ANOGEWA BONGO

Tukiwa tunaendelea na majadiliano mafupi na Alex nilimuuliza kama baada ya kuwachukua wachezaji hao utakuwa mwisho wake katika soka la Bongo, lakini niliona Alex aliguna na kusema bado ana mipango ya kuchukua wachezaji wengi zaidi.

Anasema baada ya kukutana na Kambi anataka kuhakikisha wanasaidia vijana wengi nchini kuhakikisha wanaenda kucheza soka la kulipwa Ulaya. “Sisi hatutaki kuchukua mchezaji hapa Tanzania na kumpeleka Afrika Kusini, sisi na wao tumezidiana vitu vidogo lakini Ulaya wametuzidi vitu vingi sana na ndio maana tunaangalia zaidi huko.”

Wakala huyo alifichua kwamba kuna wachezaji ambao tayari wameshapata ofa za kwenda katika akademi mbalimbali lakini wanasubiri vibali ili waende.

ANANUFAIKA VIPI?

Kama ambavyo ilivyo kwa Kambi na kwa Alex, wawili hawa wote wamesema kwa sasa hawaangalii pesa sana bali wanaangalia mchezaji kwenda sehemu ambayo ataonyesha kipaji chake ili kwenda kucheza.

Alex anasema ni ngumu mno mchezaji kutoka Bongo na kusajiliwa kwa pesa nyingi, hali hiyo imewafanya wachukuliwe wachezaji ambao wamemaliza mikataba yao na kwenda kucheza huko hoja ambayo iliungwa mkono na Kambi.

“Ni ngumu mchezaji kupata pesa ya usajili akiwa huku, ila anaweza kupata mshahara mzuri kama ambao anaupata Ally Ng’anzi, hivyo sisi tunasaidia kwanza tukiamini pesa zitakuja,” anasema.

Anaongeza kwa wachezaji ambao wanaweka pesa mbele kabla ni ngumu kufanya nao kazi kwani hata yeye hatangulizi pesa mbele akiamini zitakuja.

JAMAA ALIKIPIGA LEICESTER CITY

Kama ulikuwa unamchukulia poa Alex basi unajiongopea, Alex anafichua kabla ya kuwa na kampuni yake ya Rainbow hivi sasa aliwahi kukipiga katika klabu ya Leicester City. Alex aliniambia alisajiliwa na Leicester lakini majeraha yalikuwa changamoto katika maisha yake ya soka hali ambayo ilimfanya ajiweke pembeni.

“Nilipata majeraha ya enka na hata hivi sasa kuna vyuma nimewekewa mguuni (ananyanyua suruali na kunionyeshea), lakini nilikuwa bado natamani kucheza mpira.” Wakala huyo anasema ni rahisi kwake kumjua mchezaji kutokana yeye mwenyewe pia amecheza mpira hivyo hata katika upande wa nidhamu amekuwa hayumbishwi.

NG’ANZI NDIYE BORA KWAKE

Alex anasema kiungo Ally Ng’anzi ndiye mchezaji wake bora kwa Tanzania kutokana na amekuwa mtu wa kujifunza huku akiwa sio mzungumzaji sana.

“Ng’anzi hana mambo mengi kiukweli, ni mpambanaji muda wote anapokuwa yupo uwanjani na anaonyesha kabisa kwamba anataka kujifunza kila siku,” anasema.

Wakala huyo aliongeza kiungo huyo hana mambo mengi nje ya uwanja hivyo anaamini kabisa atakuja kuwa nyota mkubwa wa Tanzania siku za mbele.