Chipukizi Kelvin kuibeba Tanzania Chalenji Uganda

Muktasari:

Ngorongoro Heroes imeondoka leo Alhamis kwenda Uganda kushiriki mashindano ya Afrika Mashariki (Cecafa) yanayoanza Septemba 21 hadi Oktoba 5.

Dar es Salaam. Mshambuliaji wa timu ya Taifa ya vijana chini ya umri wa miaka 20 (Ngorongoro Heroes), Kelvin John 'Mbappe' amesema uzoefu wake wa mashindano ya kimataifa utakuwa chachu kwa wenzake kuipeperusha vema bendera ya Tanzania katika mashindano Chalenji kwa vijana U20.

Ngorongoro Heroes imeondoka leo Alhamis kwenda Uganda kushiriki mashindano ya Afrika Mashariki (Cecafa) yanayoanza Septemba 21 hadi Oktoba 5.

John amerejea nchini hivi karibuni akitokea Ubelgiji kukamilisha dili lake la kujiunga na timu ya vijana ya KRC Genk ya Ubelgiji anayoichezea Mtanzania Mbwana Samatta.

Kinda huyo amesema wachezaji wote wanaounda Ngorongoro Heroes ni wazuri na anaamini wataipeperusha vema bendera ya Tanzania katika mashindano hayo na kupata matokeo mazuri.

"Nina uzoefu na mechi za kimataifa za vijana hivyo nitahakikisha nawaongoza wenzangu kupambana ili tufanye vizuri na kurudi na ubingwa.

"Mashindano hayo yataniongezea baadhi ya vitu ikiwemo uzoefu, kwani najua huko nilipotoka (Ubelgiji) wananifuatilia hivyo nitajitahidi ili kuwashawishi wale wanaonihitaji wazidi kuona wamepata mtu sahihi," alisema John.