Zidane ageuka mbogo kipigo cha Real Madrid

Muktasari:

Kocha wa Real Madrid, Zinedine Zidane amesema wachezaji wake wanastahili kubeba lawama kwa kushindwa kupata ushindi dhidi ya Paris Saint Germain (PSG)

Paris, Ufaransa. Kipigo cha mabao 3-0 ilichopata Real Madrid, dhidi ya Paris Saint Germain (PSG), kimemchukiza Kocha Zinedine Zidane.

Nahodha huyo wa zamani wa Ufaransa, alisema PSG ilicheza kwa kiwango bora na wachezaji wake walizidiwa katika idara zote.

Zidane alisema kila mchezaji alichoka na hakuna aliyecheza kwa umakini. Matokeo hayo yanamuweka pabaya kocha huyo ambaye tangu aliporejea Santiano Bernabeu kwa mara ya pili,  ameshindwa kuonyesha makali.

Mchezaji mpya Edin Hazard aliyekuwa akipewa nafasi kubwa ya kutamba katika mchezo, alionyesha kiwango cha chini.

Mabingwa hao wa Ulaya mara 13, walionekana wachovu muda mrefu wa mchezo huo hatua iliyowapa nafasi wapinzani wao kucheza kwa kujiamini.

“Hakuna ubishi tulizidiwa kila idara. Walikuwa bora zaidi yetu hasa katika eneo la kiungo,”alisema nyota huyo wa zamani wa timu hiyo.

Hata hivyo, Zidane alipinga kwamba hawakufanya maandalizi ya kutosha kwa ajili ya mchezo huo.

“Jambo jema tulitengeneza nafasi za kufunga, lakini hofu yangu ni namna wachezaji wangu walivyokosa nguvu,”alisema Zidane.

Wachezaji wa viungo wa PSG Idrissa Gueye na Marco Verratti, walicheza kwa kiwango bora na kuzima mipango ya Real Madrid katika eneo la katikati.