Kiungo wa Azam, Jeba afariki dunia leo kuzikwa kesho Zanzibar

Wednesday September 18 2019

Mwanaspoti, Tanzania, Mtibwa, Kiungo wa Azam, Jeba afariki, dunia leo, kuzikwa kesho. Zanzibar

 

By Khatimu Naheka

Dar es Salaam.Kiungo wa zamani wa Mtibwa Sugar, Azam FC, Ibrahim Rajab 'Jeba' amefariki leo jioni na anatarajiwa kuzikwa kesho kijijini kwao Ndijani, Zanzibar saa saba mchana.

Taarifa zilizothibishwa na Mkurugenzi wa Ufundi wa timu ya Chuoni ya Zanzibar ambayo ndiyo klabu ya mwisho kwa marehemu kuichezea Yusuf Mohamed amesema Jeba amefariki baada ya kuugua kwa muda mrefu.

Mohamed alisema Jeba (27) tangu kuanza kwa msimu ambao tayari wamecheza mechi mbili za Ligi hakufanikiwa kucheza mechi yoyote kutokana na maradhi yake.

Kiongozi huyo alisema changamoto kubwa imekuwa marehemu hakuwa tayari kuweka wazi maradhi yanayomsumbua akisema ni siri yake.

Ingawa imekuwa ni siri, lakini taarifa ambazo hazijathibitishwa kutoka Zanzibar zinadai Jeba alikuwa akisumbuliwa na maradhi ya ini ambayo yalikuwa yakimsumbua.

Aidha Mohamed alisema Jeba alilazimika kusimama kwa muda wa wiki mbili kufuatia hali yake kutokuwa sawa ambapo msimu huu alikuwa akimalizia mkataba wake na klabu hiyo.

Advertisement

Jeba alikuwa mmoja wa viungo bora nchini ambapo alivuma akiwa na Azam na Mtibwa Sugar ya Morogoro.

Wakati akiwa Azam aliwahi kufanyiwa vipimo na kugundulika kuwa na maradhi ya moyo na kushauriwa kupumzika, lakini hakukubali akikanusha maradhi hayo.

Hata hivyo Azam ililazimika kuachana naye kutokana na ushauri wa madaktari na vipimo kuonyesha anahitajika kupumzika kwa muda mrefu.

Baadaye aliendelea kuzichezea klabu mbalimbali ikiwemo Mtibwa na kisha kurejea klabu ya Chuoni ambayo aliitumikia kwa muda mrefu.

Advertisement