Mimi Sijawahi kumuelewa uwepo wa Said Ndemla ndani ya Simba

Muktasari:

Simba mara zote imekuwa bize kununua mastaa wa kigeni katika eneo hilo. Staa wa ndani ambaye anapata nafasi katika eneo hilo ni Jonas Mkude zaidi.

MCHEZAJI ambaye sijawahi kumuelewa maishani ni Said Ndemla. Anachezea Simba. Huwa namuona mara chache uwanjani akiwa na jezi ya Simba. Kuna nyakati huwa namuona na kuhisi kwamba ni kiungo maridadi. Anapiga chenga maridadi. Ana tabia ya kupiga mashuti. Ana tabia ya kujichangamsha uwanjani. Napenda wachezaji wa namna hii. Anacheza huku akiwa anataka jambo fulani litokee.
Tatizo kubwa ni kwamba sijawahi kumfaidi kwa sababu simuoni uwanjani mara nyingi. Ninachojua, kwa umri wake, anahitajika kucheza zaidi uwanjani kuliko kukaa katika benchi au jukwaani.
Nadhani pale Simba kuna viungo wengi ambao labda makocha wanaopita Simba wanaamini kwamba wana uwezo kuliko Ndemla. Haishangazi kuona anakalia benchi na mashabiki huwa wanasahau uwepo wake klabuni.
Kuna mambo mawili yanayojichanganya kuhusu Ndemla na Simba yake.
Kwanza kabisa Simba haitaki kumuacha. Labda wanahisi kwamba ana kitu kikubwa miguuni na huenda siku za usoni akawa na msaada mkubwa kwao.
Nilishangaa wakati Simba iliponunua viungo wa nguvu klabuni na bado ikaamua kumuongezea mkataba mpya Ndemla.
Inawezekana kuna kitu ambacho wanakiona ambacho watu wengine hawakioni. Lakini mbona hawamtumii wala kumuweka katika hesabu zao mara kwa mara?
Simba mara zote imekuwa bize kununua mastaa wa kigeni katika eneo hilo. Staa wa ndani ambaye anapata nafasi katika eneo hilo ni Jonas Mkude zaidi. Mwingine ambaye amekuwa akicheza lakini sio mchezaji wa kudumu ni Mzamiru Yassin. Mwingine ambaye amekuwa akicheza zaidi ni Hassan Dilunga. Hakuna nafasi kwa wengine wala kwa Ndemla ambaye namzungumzia hapa.
Hata hivyo, Simba bado wapo na Ndemla na inapofika wakati wa usajili wanaendelea kuwa naye. Kinachochekesha ni kwamba ikifika wakati wa usajili watani zao Yanga wanaanza kuchafua hali ya hewa kwa kujidai wanamtaka Ndemla.
Lakini kwa upande wa Ndemla mwenyewe nadhani hana hata hofu.
Anapenda tu kuwa mchezaji wa Simba. Hana presha hata kama hachezi. Sidhani kama anachukia kutocheza.
Katika umri alionao, vijana wenzake wengi wanacheza kwingineko hata kama sio Simba. Lakini yeye hana presha. Ameridhika kuwa mchezaji wa Simba.
Kwa kipaji chake kama akichezeshwa mechi kumi mfululizo na Simba anaweza kurudisha kujiamini na akawa mchezaji mwingine kabisa tofauti kabisa na huyu ninayemzungumzia hapa.
Lakini pia, hata kama sio Simba Ndemla angeweza kuondoka na kwenda katika timu ambayo atacheza mara nyingi zaidi na kuibuka kuwa imara zaidi.
Kuna wachezaji wa namna hii ambao walionekana wa kawaida katika timu kubwa lakini wakaenda kwingine na kuibuka kuwa wachezaji imara zaidi na kisha wakarudi katika klabu kubwa.
Mmojawapo ni huyu hapa Hassan Dilunga. Pale Yanga walijaa mastaa katika eneo la kiungo akina Thaban Kamusoko na Haruna Niyonzima. Nafasi yake ikapotea. Akaamua kuondoka.
Dilunga akaibuka kuwa msumbufu zaidi katika timu ndogo na mwishowe Simba wakanyoosha mikono na kumchukua.
Hata njia ya Ndemla kwenda Yanga au Azam inaweza kuwa ya staili hii. Anaweza kwenda zake Mtibwa akaibuka kuwa mchezaji bora zaidi na kisha akarudi mjini katika timu kubwa akiwa amekomaa. Ni bora zaidi kuliko kukaa jukwaani kama mtazamaji kila mwisho wa wiki.
Kitu kikubwa kinachowalemaza wachezaji wetu na kuamua kubakia katika klabu kubwa ni mateso makubwa wanayopata wakiwa katika klabu nyingine ndogo nje ya Simba, Yanga na Azam.
Wanajua wakienda katika klabu kama Ndanda au zile za Jeshi wanaweza kusota. Hakuna kupanda ndege, hakuna kushabikiwa sana mitaani na mashabiki.
Wasichofahamu ni kwamba kama wakijiamini wanaweza kurudi katika klabu kubwa na kufanya mambo makubwa kama ambavyo Dilunga alifanya na anaendelea kuheshimika licha ya kuonekana mchezaji wa kawaida akiwa na Yanga.
Kitu kingine ambacho kinaniacha mdomo wazi kwa Ndemla ni ukweli kwamba amewahi kwenda nje kujaribu bahati yake.
Alikwenda Sweden. Mtu ambaye alimpeleka anadai kwamba Ndemla alikubalika. Sijui kitu gani kimeendelea hadi sasa kimemfanya aendelee kuwepo nchini.
Huwa naamini kwamba wakati mwingine hatupati majibu kuhusu safari za wachezaji wetu wanapokwenda katika majaribio.
Wachezaji wetu huwa wanaondoka kwa mbwembwe kwamba wanakwenda kufanyiwa majaribio, basi unasikia walifuzu, baadaye unasikia kimya.
Mwisho wa siku, kwa vyovyote ilivyo, nadhani washauri wa Ndemla wamshauri acheze soka. Awe mchezaji mshindani asiyekubali kukaa benchi.
Inawezekana Simba wanamuweka benchi kwa sababu hawaoni juhudi zake za kutafuta nafasi akiwa mazoezini lakini wanakiri kwamba ana kipaji kikubwa.
Washauri wake wamwambie awanie nafasi yake kwa nguvu zote maradufu. Kama hilo likishindikana kutokana na Simba kuwa na wachezaji mahiri na wanaojituma zaidi katika nafasi hiyo basi sio mbaya akajaribu kwingineko. Anaweza kurudisha uwezo wake wa kujiamini na anaweza kurudi katika klabu kubwa kwa heshima.
Mpaka sasa sijawahi kumuelewa Ndemla. Kila nikijaribu kumtafuta nimuone simuoni na namuona ameridhika na maisha anayoishi sasa hivi. Mchezaji lazima uchukie kutocheza. Mpira ni maisha yako. Mchezaji lazima upambane kwa ajili ya kuwa kazini kila siku. Kwa mchezaji, kazini ni ndani ya uwanja katika nyasi na sio jukwaani.
Kitu kibaya zaidi katika kazi ya mwanasoka ni pale ambapo timu inapocheza vizuri huku ikishinda bila ya wewe kukumbukwa. Ni kitu kibaya katika maisha ya soka kama vile ambavyo mfanyakazi wa kawaida anapoweza kwenda likizo na pengo lake lisionekane.
Ndemla lazima ajiwekee malengo kwamba msimu huu uwe wa mwisho kwake. Ama atinge katika kikosi cha kwanza cha Simba au awe mchezaji wa kudumu katika klabu nyingine ya Ligi Kuu ambayo inashindana na itaonyesha kipaji chake maridhawa.
Mfano ni KMC au Mtibwa Sugar ambayo ndio kwa kiasi kikubwa ilimrudisha tena katika chati rafiki yake Dilunga. Huu ni ukweli ambao kama angekuwa mdogo wangu ningemwambia aumeze.
Kwa ninavyoitazama Simba siwezi kuilaumu kwa sababu haina cha kupoteza. Kama wanaweza kumlipa stahiki zake huku akikaa benchi na kutimiza idadi ya wachezaji wa mazoezi basi kwao sio shida.
Ni mchezaji binafsi ndiye anayepaswa kuangalia mwelekeo wake.
Mwisho wa kila kitu mchezaji atazeeka lakini Simba itaendelea kuwa pale pale na kununua wachezaji wengine kwa miaka mingi ijayo.
Hakuna mchezaji mkubwa kuliko klabu.