Njaa ilivyopukutisha mabondia uzito wa juu nchini

Muktasari:

Kati ya mabondia 1049 wa uzani wa juu wanaotambulika duniani wakiongozwa na Ruiz Jr, Watanzania wawili pekee ndiyo wako katika orodha hiyo ambao ni Alphonce Mchumiatumbo ambaye yuko nafasi ya 496 na Victor Mashaka wa 746.

Dar es Salaam. Umewahi kujiuliza ule mzuka wa mashabiki wa ndondi kwenye mapambano ya mabondia wa uzani wa juu (heavy weight) nchini umepotelea wapi miaka ya hivi karibuni?.
Iko wapi ile ‘team’ iliyokuwa ikimsapoti Chuku Duso akizichapa na Joseph Marwa, Awadh Tamim dhidi ya Ashrafu Suleiman au ile iliyofunga mtaa na kusimamisha jiji Koba Kimanga akizichapa na Nasoro Michael?
Zile enzi za mashabiki kukesha wakisubiri kushuhudia laivu Mike ‘Iron’ Tyson akimchakaza Evander Holyfield au Francois Botha akichezea kipigo ‘hevi’ cha Lennox Lewis.
Waliibuka pia kina Vladimir Klitschko na kaka yake Vitali Klitschko, David Haye na sasa kina Deontay Wilder ‘Bronze Bomber’. Tyson Fury, Andy Ruiz Jr na Anthony Joshua ‘AJ’ na wengine wengi wanazidi kufanya vizuri duniani katika uzani wa juu.
Kati ya mabondia 1049 wa uzani wa juu wanaotambulika duniani wakiongozwa na Ruiz Jr, Watanzania wawili pekee ndiyo wako katika orodha hiyo ambao ni Alphonce Mchumiatumbo ambaye yuko nafasi ya 496 na Victor Mashaka wa 746.
Hapa nchini uzani huo una mabondia wanne, wakiongozwa na  Mchumiatumbo, Mashaka (namba 2),  Salum Habibu na John Haule ambao wote watatu wako kwenye ubora nchini japo hawatambuliki katika mtandao wa ngumi wa dunia (boxrec).
Awali walikuwapo mabondia wa uzani wa juu kama Zollah D na wengine wengi lakini sasa hawasisiki tena, wamepotea hakuna hamasa ya mapambano ya uzani wa juu nchini.

Mabondia watoboa siri
Bingwa wa zamani wa uzani wa juu Afrika Mashariki na Kati, Awadh Tamim anasema tatizo ni mtazamo, watu wengi nchini walifikiri sifa ya kuwa ‘hevi’ lazima uwe kibonge wakati si lazima .
“Bondia wa uzani wa juu anatengenezwa, japo sifa kuu kwanza lazima uwe na afya nzuri, ule vizuri na uwe na uwezo wa kufanya mazoezi makali, lakini baadhi ya waliokuwa wakiingia ni bondia tu ambaye amenenepa.
“Ngumi ni moyo, ukiingia tu kwa kuwa una sifa ya kuwa mnene lazima uishie njiani, ngumi ni ngumu hivyo ili kucheza lazima pia uwe na kipaji, roho ngumu, uvumilivu na malengo ambayo mwishoni utaona matunda ya kazi unayoifanya.
Anasema bondia wa uzito wa juu lazima uwe na kilo za kutosha, ale vizuri na kushiba ili aweze kufanya mazoezi na sio kuunga unga, ili kufanikisha hilo lazima uwe na meneja na mtu wa kukupromoti.
“Kama huna promosheni ambayo itakusimamia kuanzia chakula, mazoezi, vifaa lazima ukwame, Tanzania kuwa bondia hevi ni ngumu sana kama hakuna uwekezaji, huwezi kuwa na njaa ukastahimili kurusha ngumi za uzoto wa juu,” anasema Tamim, ambaye sasa anaishi Sweden.
Mchumiatumbo anasema mikakati ya kiuongozi na kukosa upinzani kwa mabondia waliopo ndiyo kumechangia kuadimika kwa mabondia wa uzani wa juu nchini.
“Kumhudumia bondia wa uzani wa juu ni gharama, wakati Ashraf na Awadh wanatamba nchini, kampuni ya Aurora ilikuwa ikiwa promoti, baada ya hapo hakuna promosheni ambayo imeendelea kuwakuza mabondia wa uzito wa juu,” anasema.
Bondia Koba Kimanga anasema mabondia wa uzani wa juu wameadimika nchini kutokana na kizazi cha sasa lakini pia wale wachache wenye miili ya kucheza uzani wa juu, hawajitokezi.
“Mabondia wa uzani wa juu wegi wao wanatengenezwa, lakini mfumo wa ngumi zetu sasa ni kama umewapa kisogo mabondia hao, hakuna anayekumbuka kuwatengeneza, lakini hawa ni bidhaa adimu ambayo kama tukiwatengeneza vizuri hata wanne tu, wakaingia anga za kimataifa tutafika mbali,” anasema.
Bondia Nasoro Michael ambaye alikuwa tishio kwenye timu ya Taifa ya ngumi za uzito wa juu miaka ya nyuma anasema si Tanzania pekee, hata duniani ile hamasa ya mabondia wa uzani wa juu imepungua baada ya Mike Tyson kustaafu.
“Alipoibuka Floyd Maywether akatikisa dunia, kibao cha amsha amsha ya mabondia wa uzani wa juu nacho kikageukia kwenye uzani wa kati, ni kama tunakwenda kwa kupokezana kijiti.
“Tanzania pia aliibuka Francis Cheka (uzani wa kati) na sasa Hassan Mwakinyo (super welter) ni kama mapinduzi yamefanyika, japo kwenye uzani wa juu duniani sasa ndipo ameibuka Anthony Joshua ambaye ametengenezwa upya na ile hamasa kama wakati wa Tyson imeanza kurejea,” anasema.

Nini kifanyike?
Kocha Habibu Kinyogoli anasema ili kurejesha hamasa ya mabondia wa uzani wa juu, kunapaswa kuwepo na promosheni nyingi ambazo zitawasimamia mabondia.
Anasema changamoto kubwa iko kwenye kuwasimamia mabondia hao kutokana na mfumo wa kimichezo uliopo nchini ambapo michezo mingi haina udhamini.
“Kama tukifanikiwa kuwa na promosheni nyingi kwenye boxing, hakuna shaka ile hamasa ya miaka ya nyuma itarejea upya.