Ndayiragije atimiza ndoto ya Miraji Athuman kucheza Stars

Muktasari:

Kocha Ndayiragije alitangaza kikosi cha wachezaji 25 wa Stars kitakachocheza dhidi ya Sudan kusaka tiketi ya kufuzu kwa CHAN2020 Cameroon, huku Athuman akiitwa kwa mara ya kwanza.

Dar es Salaam. Uamuzi wa kocha wa Taifa Stars, Etienne Ndayiragije kumjumuisha winga wa Simba, Miraji Athuman katika kikosi hicho kimetimiza ndoto ya muda mrefu ya mchezaji huyo.

Kocha Ndayiragije alitangaza kikosi cha wachezaji 25 wa Stars kitakachocheza dhidi ya Sudan kusaka tiketi ya kufuzu kwa CHAN2020 Cameroon, huku Athuman akiitwa kwa mara ya kwanza.

Athuman ameonyesha kiwango cha juu katika kikosi cha Simba dhidi ya JKT Tanzania na Mtibwa Sugar na kufunga bao moja moja kila mechi.

Baada ya Athuman kusikia jina lake limejumuishwa katika kikosi cha Stars, alisema ndoto yake ya muda mrefu kuichezea nchini yake imetimia.

Alisema imemuongezea kujiamini kuona kazi yake anayofanya ndani ya Simba, inatazamwa na wengi hivyo anaona anaweza akafanya makubwa zaidi.

"Ilikuwa ndoto yangu kuichezea Taifa Stars, imenipa moyo kuona kocha ameniita ndani ya kikosi hicho, kati ya wachezaji wengi ambao tunacheza ligi kuu Bara"

"Imenipa chachu ya kuendelea kujituma na kupambana kuhakikisha nafika mbali zaidi ya hiki ninachokifanya kwa sasa,"alisema Miraj.