Buswita: Yanga imtazame Kamusoko kwa jicho la tofauti

Muktasari:

Yanga itarudiana na Zesco nchini Zambia katika mchezo wa kusaka kufuzu kucheza hatua ya makundi ya Ligi ya Mabingwa.

Dar es Salaam.Kiungo wa zamani wa Yanga, Pius Buswita amewataka wachezaji wa timu hiyo kujipanga vilivyo kumzuia Thaban Kamusoko katika mchezo wao wa marudiano dhidi ya Zesco ya Zambia.

Buswita alisema wachezaji waliocheza na Kamusoko wakiwa Yanga ni Kelvin Yondan na Deus Kaseke, amewataka wawe viongozi wa wengine kuwaelekeza namna ya kwenda kukabiliana na staa huyo.

Buswita alisema pamoja na Kamusoko kuondoka Yanga, haimanishi ameshuka kiwango, ni mchezaji ambaye sifa yake ni kuituliza timu na ikacheza kupitia yeye.

"Kiukweli Kamusoko ni mtu hatari, lazima wachezaji wa Yanga walijue hilo, nakumbuka wakati nacheza naye alikuwa anauwezo wakutuliza presha ya timu pia ni fundi wa pasi na mashuti.

"Kuna wakati wachezaji tulikuwa tukitoka mchezoni anatutuliza na tunacheza kupitia yeye, lazima wakawe makini naye na tayari ameionyesha cheche zake hapa Dar es Salaam."

Anaamini Yanga ina nafasi kubwa ya kwenda kushinda mchezo huo, akiwatia moyo wachezaji wa kikosi hicho kwamba wajiamini na kuwa kitu kimoja.

"Mpira ni dakika 90 haiwezekani eti kwa sababu wametoka sare basi Yanga itakwenda kushindwa ugenini, naamini wanaweza wakafanya maajabu dhidi ya Zesco huko Zambia," alisema Buswita.