Gor Mahia ni aibu tupu ushiriki wake Ligi ya Mabingwa Afrika

Tuesday September 17 2019

Gor Mahia, Tanzania, Kenya, aibu tupu, ushiriki wake, Ligi ya Mabingwa, Afrika

 

By Thomas Matiko

Dar es Salaam. MATATIZO ya mabingwa watetezi wa Ligi Kuu nchini, Gor Mahia yaliendelea kuwafuata kule ugenini Algeria baada ya kulimwa mabao 4-1 na wenyeji hao kwenye mechi ya raundi ya pili ya kufuzu hatua ya makundi ya dimba la CAF Champions League.
Gor ambao nusura wasusie mechi hiyo kwa kukosa fedha za kununua tiketi za ndege kusafiri, hatimaye walihabatika na kuwasili mjini Algers Jumamosi, kabla ya kuchuana na wenyeji siku iliyofuata.
Kwa wiki nzima miamba hao walikuwa wakiombaomba wasaidiwe fedha za usafiri bila ya mafanikio. Waliishia kufanya mchango wakilenga kupata Sh5 milioni kugharimia tiketi hizo ila waliishia kuchangisha Sh1,5 milioni pekee baada ya wageni waalikwa Raila Odinga na gavana Mike Sonko kususia.
Hata hivyo, Raila ambaye ni mlezi wa klabu alijitahidi na kuishawishi Wizara ya Michezo iliyokuwa imegoma kuwasaidia hapo awali, kuwanunulia tiketi hizo.
Waliondoka nchini usiku wa Ijumaa na kufika Algeria Jumamosi. Mechi ikapigwa Jumapili na wakaishia kufedheheshwa kwa kufungwa magoli 4-1, ishara tosha huenda safari yao ya kutinga hatua ya makundi, imefikia kikomo labda tu itokee miujiza kwenye mechi ya marudio mjini Nairobi.
Mechi hiyo ilianza kwa vishindo Mwarabu akipata bao la kwanza dakika ya 16 kupitia Mohamed Rabie Meftaah aliyemaliza pasi safi iliyotika kwa Mouaid Ellafi baada ya chenga za maudhi.
Dakika moja kabla ya mapumziko, kipa Mtanzania David Mapigano Kisu alifanya blanda kwa kumtega Meftaah kwenye kisanduku na kusababisha penalti iliyotiwa kimiani kwa bao la pili. Sekendu chache tu kabla ya kipenga hicho cha mapumziko kupulizwa, Zakaria Bencha aliachia shuti kali iliyopinda na kuzama wavuni baada ya kugonga milingoti yote miwili.
Katika kipindi cha pili, Gor walijaribu kuwaletea presha na jitihada zao zilizaa matunda pale mpira wa krosi ya kona kutoka  kwa Charles Momanyi iliishia kuugonga mkono wa Tahar Benkhalifa na wakazawadiawa penalti, nahodha Kenneth Muguna akautia kimyani.
Hata hivyo, Alger walijibu mapigo tena kwa Zakaria kupachika bao la nne, baada ya blanda nyingine ya kipa Mapigano. Zakaria aliachia kombora kali alilolipangua Mapigano kuelekea alikokuwa straika huyo ambaye hakusita kuisukuma wavuni kwa mara nyingine.

Advertisement