Mkongwe Nizar aiongoza Pamba kuichapa Stand United

Monday September 16 2019

Mwanaspoti, Tanzania, Nizar aiongoza, Pamba, kuichapa Stand United, Ligi daraja, kwanza

 

By Saddam Sadick na Masoud Masasi

Mwanza. Pamba FC imeanza vyema Ligi Daraja la Kwanza kwa kuichapa Stand United mabao 3-1 katika mchezo uliopigwa leo Septemba 16 kwenye Uwanja wa Nyamagana jijini Mwanza.

Katika mchezo huo uliokuwa na ushindani, Pamba ilionyesha nia ya kuhitaji ushindi na kufanikiwa kubaki na pointi tatu muhimu.

Kipindi cha kwanza Pamba walionekana kutulia na kutengeneza mashambulizi ambayo kimsingi yaliweza kuwapa faida ya mabao mawili yaliyowekwa kambani na Amos Matai dakika ya 12 na Nizar Khalfan dakika ya 32.

Kipindi cha pili Stand United walirejea kwa kasi na kufanikiwa kuandika bao la kujifariji dakika ya 47 lililofungwa na Miraji Salehe na wakati hekaheka ikiendelea, Saady Kipanga akaifungia bao la tatu Pamba akiunganisha kwa kichwa krosi ya Rashid Njete.

Bao hilo lilionekana kuwaamsha zaidi Stand United waliokuwa na kundi kubwa la mashabiki na kuanza kushambulia,lakini mambo yaliwawia magumu katika kusawazisha mabao hayo.

Advertisement