Simba bado yaweweseka kuondolewa Ligi ya Mabingwa na UD Songo

Monday September 16 2019

Simba yakiri, Mwanaspoti, UD Songo, yaweweseka, kuondolewa, Ligi ya Mabingwa, Tanzania

Beki wa kushoto wa Simba, Mohammed Hussein 'Tshabalala' akiwa anawapiga picha wenzake wakati wa mazoezi ya timu hiyo leo asubuhi kwenye Uwanja wa Gymkhana, Dar es Salaam. 

Dar es Salaam.Meneja wa timu ya Simba, Patrick Rweyemamu amekiri kutolewa katika hatua ya awali ya Ligi ya Mabingwa Afrika bado kinawasumbua, lakini wanashukuru wameanza Ligi Kuu Bara kwa kushinda mechi mbili mfululizo.

Patrick amesema bado kiakili wachezaji na viongozi hawapo vizuri kutokana na kutolewa mapema katika mashindano hayo makubwa Afrika.

Simba imetolewa hatua ya awali ya Ligi ya Mabingwa Afrika na UD Songo ya Msumbiji baada ya kutoka sare ya bao 1-1 hivyo kuondolewa kwa bao la ugenini.

"Baada ya kuwapa wachezaji wetu mapumziko ya siku mbili Jumamosi na Jumapili leo Jumatatu tumerejea mazoezini kujiandaa na mchezo dhidi ya Kagera Sugar ambao umepangwa kufanyika Septemba 26.

"Tunashukuru tumeanza ligi vizuri kwa kushinda mechi zote mbili dhidi ya JKT Tanzania na Mtibwa Sugar licha ya kwamba bado kiakili wachezaji na viongozi wote hatuko vizuri.

"Kitendo cha kutolewa hatua ya awali Ligi ya Mabingwa Afrika kimetusononesha, lakini tunakomaa kuhakikisha tunasahau hayo na kuendelea kupambana katika Ligi," alisema Patrick.

Advertisement

Patrick alisema wachezaji wote mazoezini wako katika hali nzuri isipokuwa John Bocco ambaye anaendelea na mazoezi maalum kutokana na kuwa majeruhi.

Bocco aliumia msuli wa paja katika mchezo wa Ngao ya Jamii dhidi ya Azam.

Advertisement