Mtendaji Mkuu mpya Simba atangaza mambo matatu mazito

Muktasari:

Mazingiza ametaja mambo matatu makuu ambayo ataanza nayo ndani ya Simba ambayo ni kutengeneza sura makini ya uongozi akisuka Sekretarieti inayojitegemea na kuongozwa kwa weledi ili kuipeleka klabu hiyo mbali zaidi. Pili ni kuibuka na kuendeleza vipaji vya wachezaji kuanzia ngazi za chini ikiwa ni pamoja na kuunda timu za vijana za rika mbalimbali kupitia mfumo wa wazi na unaozingatia misingi ya soka.

DESEMBA 3, mwaka 2017 wakati bilionea Mohamed Dewji (MO) akitangazwa mshindi wa zabuni ya kuwekeza ndani ya Simba, alizungumza mambo 10 yaliyowapa mzuka mashabiki wa klabu hiyo.
Ilikuwa tukio ambalo wanachama na mashabiki wengi wa Simba waliamini linakwenda kuondoa unyonge mbele ya watani zao wa jadi, Yanga ambao walikuwa wametawala soka la Tanzania wakibeba taji la ubingwa wa Ligi Kuu Bara kwa misimu mitatu mfululizo.
Miongoni mwa ahadi ambazo MO alizitoa ni pamoja na kuifanya Simba kuwa na miundombinu ya kisasa ikiwemo viwanja vya mazoezi na mechi. Aliahidi kuanza na viwanja viwili kimoja cha nyasi bandia na kingine nyasi asilia.  Pia, aliahidi kuifanya Simba kuwa klabu ya kisasa yenye timu za umri mbalimbali kuanzia chini ya miaka 14, 16 na 18 na lengo ni kuwakuza na kuwauza vijana hao kwenye mataifa mbalimbali.
Katika kuonyesha yuko siriasi, MO pia alitangaza atahakikisha brandi ya Simba inakuwa kimataifa na kuwatumia mashabiki kama wateja wa uhakika wa kununua bidhaa mbalimbali za Simba ikiwemo jezi, vishika funguo, maji kama ilivyo kwa klabu zingine kubwa barani Ulaya.
Sasa ni takriban mwaka mmoja na miezi tisa, mikakati hiyo ya MO imechukua sura mpya kwa kumpata mtu mwenye malengo na mipango yake katika uendeshaji wa klabu hiyo.
Jana Simba imemtambulisha Mtendaji Mkuu mpya, Senzo Mazingiza ambaye anachukua nafasi ya Crescentius Magori aliyetangaza kung’atuka miezi kadhaa iliyopita ili kutoa fursa kwa wengine kushika kijiti chake.
Kama ambavyo huko nyuma Mwanaspoti lilivyomwelezea Mazingiza, raia wa Afrika Kusini kuwa ni mtu wa mpira na mwenye rekodi zake tamu akipata nafasi ya kuziongoza klabu kubwa kama Orland Pirates na Platnumz Stars, kwa mikakati yake aliyoieleza jana wakati akitambulishwa rasmi basi Simba haitakuwa klabu ya kuigusa kabisa.
Mazingiza ametaja mambo matatu makuu ambayo ataanza nayo ndani ya Simba ambayo ni kutengeneza sura makini ya uongozi akisuka Sekretarieti inayojitegemea na kuongozwa kwa weledi ili kuipeleka klabu hiyo mbali zaidi. Pili ni kuibuka na kuendeleza vipaji vya wachezaji kuanzia ngazi za chini ikiwa ni pamoja na kuunda timu za vijana za rika mbalimbali kupitia mfumo wa wazi na unaozingatia misingi ya soka.
“Hili ngoja nieleze kidogo, mashabiki wengi wakiizungumzia klabu wanaangalia tu timu kubwa, lakini kwangu ni tofauti kabisa. Klabu ni pamoja na kuwa na vikosi vya vijana, timu ya wanawake yaani timu zote zinazoundwa hadi kufikia ya wakubwa hiyo ndiyo tunaita klabu na vikosi vyote hivyo lazima viundwe kwa umakini,” alisema Mazingiza.
Jambo lingine ambalo Mazingiza amelielezea ni kuifanya Simba kuwa klabu inayojitambulisha kibiashara ndani ya Afrika na Duniani ikiwa ni pamoja na kuuza bidhaa zake kwenye mataifa tofauti.
“Tunahitaji kuipeleka Simba kwenye uso wa kibiashara duniani, kama nilivyosema Simba sio klabu kubwa tu Tanzania ni Afrika na ukubwa wa jina lake lazima uendane na ukubwa wa kibiashara zake. Hapo ndio tutakuwa tumejenga klabu yenye mafanikio Afrika na duniani.
“Nilifika hapa nchini mapema ila sikutaka kujitangaza, nilijificha kidogo ili kuangalia mambo yalivyo. Niliona mashabiki walivyojaa uwanjani katika ile Simba Day, ilikuwa ni balaa hata kule kwetu niliporudi mabosi wa Orlando Pirates na Mamelodi Sundowns waliniuliza kuhusu mashabiki.
“Lakini, jambo muhimu hapa ni kugeuza ule umati wa mashabiki zaidi ya 60,000 kuwa wateja wa Simba, ni lazima mashabiki watambue na kuifikiria Simba katika kila matumizi yao ya kifedha kila siku na hili ndio litakuwa jukumu letu,” alisema.

Hapa ni mastaa na mataji
Mazingiza alisema ni hatua mbaya kwa Simba kuondolewa mapema kwenye Ligi ya Mabingwa Afrika, lakini mikakati yao kwa sasa ni kuchukua mataji yote ya ndani yaliyosalia.
Alisema mbali na hilo, pia atahakikisha Simba inapata wachezaji wenye viwango vya juu lakini, mafanikio hayo hayawezi kutokea kwa haraka na yanahitaji ushirikiano.
“Nimeiona timu ni nzuri lakini huko mbele tunahitaji wachezaji bora zaidi, haya mambo yote hatakuja mara moja inahitaji muda hata TP Mazembe haikuchukua kombe la Afrika kwa haraka.”

Wazawa sita wapigwa chini
Awali, Magori alisema mchakato wa kumpata Mazingiza haukuwa mfupi na kwamba katika watu nane walioomba Watanzania walikuwa wawili tu.
“Mchakato uliongozwa na kamati maalum ambayo ilikuwa chini yangu na waliomba watu nane, katika hao sita ni wazawa wawili wakiwa wageni katika hao wageni alikuwemo pia mmoja kutoka Amerika