Wazee wa zengwe Old Trafford wapo kimyaaa kama hawaoni vile

Muktasari:

Kuna mtu anaitwa Roy Keane, mwingine anaitwa Paul Scholes, kuna Gary Neville na mdogo wake, Phil Neville, kuna Paul Ince. Wapo wengi tu ambao walitamba katika kikosi cha United utawala ule wa Sir Alex Ferguson. Hawa bado wana mamlaka na sauti kubwa ndani ya Old Trafford.

PALE Old Trafford kuna wazee wangu wa zengwe. Huwa wananifurahisha sana. Kuanzia utawala wa David Moyes hadi huu wa Old Gunnar Solskjaer wao kazi yao ni kupika mizengwe tu, lakini kwa sasa wapo kimya.
Kuna mtu anaitwa Roy Keane, mwingine anaitwa Paul Scholes, kuna Gary Neville na mdogo wake, Phil Neville, kuna Paul Ince. Wapo wengi tu ambao walitamba katika kikosi cha United utawala ule wa Sir Alex Ferguson. Hawa bado wana mamlaka na sauti kubwa ndani ya Old Trafford.
Wanakaa katika makochi ya SkySport na kukosoa vikali. Wanatamba kwa sababu katika utawala wao wa soka pale Old Trafford walifanya mambo makubwa uwanjani. Mashabiki wanawaheshimu kupita kiasi na kauli zao huwa zinaheshimiwa pia. Makocha waliokuja baada ya Sir Alex wamepata tabu pale. Lakini sasa wameingia mtegoni. Aliyepewa nafasi ya kukalia kiti ni mwenzao. Walicheza naye. Nadhani wanasita kuanzisha mashambulizi. Kama angekuwa kocha mwingine mashambulizi yangekuwa yameanza.
United baada ya kumchapa Chelsea mechi ya mwanzo amechemsha katika mechi tatu zilizofuata dhidi ya Wolves, Palace na Southampton. Ilitosha kwa kina Keane kufungua midomo lakini naona wamekaa kimya kwa sababu ni mwenzao. Mpaka sasa ni mechi nne zimechezwa na kila timu lakini United imeshaachwa pointi saba na viongozi wa Liverpool ambao ni wapinzani wao wakubwa katika soka la Kiingereza kuliko watani wao Manchester City. Kama hili lingemtokea Jose Mourinho nadhani sasa hivi kelele zingekuwa zimeanza. Kwa rafiki yao bado wako kimya na nadhani hata wazee wa zengwe wakiamka, basi kelele zao zitaanza kwa wachezaji zaidi na watamuweka kando kidogo rafiki yao. Wanajua kufeli kwa Solskjaer ni kufeli kwao wote. Muda mrefu sasa walikuwa wanatamani United ishikiliwe na mchezaji wa kizazi chao wakiamini anajua utamaduni na mila za klabu. Wasichojua ni kwamba mpira umebadilika na hilo sio jambo muhimu tena klabuni hapo. Naiona timu ikienda katika mikono ya mtu anayeitwa Mauricio Pochettino. Sidhani kama Solskjaer atafika Novemba mwaka huu. Sina uhakika sana. Anajaribu kutumia mbinu za kizamani katika soka la kisasa kama kuwajaribu makinda kina Mason Greenwood. Sioni kama watamkomboa.