Simba yachora ramani ya ubingwa Ligi Kuu Bara mapema

Muktasari:

Mpango wa Simba ni kumaliza ligi mapema kwa maana ya kupata ushindi kwenye mechi zake za nyumbani na ugenini ili Yanga wakimaliza anga za kimataifa, wanaikuta Simba inakaribia kutangaza ubingwa kama ilivyokuwa Manchester United ya wakati ule wa Sir Alex Ferguson.

MABINGWA watetezi wa Ligi Kuu Bara, Simba wanaendelea kujifua kwenye viwanja vya Gymkhana, Dar es Salaam ikiwa ni maandalizi ya kimkakati kwa ajili ya kusaka ubingwa kwa mara ya tatu mfululizo.
Tayari, Simba imeondolewa kwenye Ligi ya Mabingwa Afrika ikiwa hatua ya awali kabisa na sasa mkakati wao ni kumaliza biashara mapema, kwa maana ya kubeba ubingwa wakati huo Yanga wakiendelea na harakati za kimataifa.
Yanga bado iko kwenye Ligi ya Mabingwa Afrika na Jumamosi ijayo watakuwa na kibarua dhidi ya Zesco United. Kama watashindwa kupata matokeo nyumbani na ugenini, na Zesco kupata nafasi ya kusonga mbele, basi Yanga itaangukia kwenye michuano ya Kombe la Shirikisho Afrika. Yaani bado wataendelea kutesa kimataifa tu.
Hata hivyo, mpango wa Simba ni kumaliza ligi mapema kwa maana ya kupata ushindi kwenye mechi zake za nyumbani na ugenini ili Yanga wakimaliza anga za kimataifa, wanaikuta Simba inakaribia kutangaza ubingwa kama ilivyokuwa Manchester United ya wakati ule wa Sir Alex Ferguson.
Wanachokifanya kwa sasa bechi la ufundi la Simba na mabosi wa klabu hiyo, ni kuchora ramani ya ubingwa kwa kunasa alama 15 kwenye mechi zao tano zijazo kuanzia ile ya raundi ya pili.
Ratiba inaonyesha hadi kufikia mwezi Desemba, Simba itakuwa imecheza mechi saba ngumu ambazo mbili watakuwa nyumbani katika Uwanja wa Taifa au Uhuru na tano watakuwa ugenini.
Ramani ya Simba kurejea anga za kimataifa msimu ujao itaanza Septemba 17, ambapo watakipiga na Mtibwa Sugar katika mechi ya pili ya ligi huku rekodi za mechi tatu zilizopita katika ndimba la Taifa zikionyesha kuwa Simba wameshinda mechi mbili na kutoka sare moja.

NA MTIBWA
Rekodi zinaonyesha Simba katika msimu uliopita kwenye mechi za Dar es Salaam - ile iliyochezwa Septemba 16 walishinda mabao 3-0 wakati msimu wa 2017-18 walitoka sare 1-1 na msimu wa 2016-17 walishinda mabao 2-0.
Kwa maana hiyo katika mechi tatu zilizopita dhidi ya Mtibwa Sugar ambazo zimechezwa Dar es Salaam, wamewafunga mabao sita wakati wao wakiruhusu nyavu zao kutikiswa kwa kufungwa bao moja.
Baada ya kumalizana na Mtibwa Sugar, Septemba 22 watakuwa na kibarua kingine tena nyumbani kucheza na Lipuli ambao tangu wamepanda daraja misimu miwili iliyopita wamekutana na Simba mara mbili na zote ziliisha kwa sare.
Msimu wa kwanza Lipuli walipopanda Ligi Kuu  2017-18 walitoka sare 1-1 na Simba katika Uwanja wa Uhuru huku ule uliopita katika mechi ya Dar es Salaam, walitoka tena suluhu.
Baada ya hapo kikosi cha Simba kitaanza safari hadi Bukoba ambapo wakiwa  umbali wa kilomita 1,433 watakipiga na Kagera Sugar kwenye Uwanja wa Kaitaba, Oktoba 3.
Rekodi zinaonyesha katika mechi tatu zilizopita ambazo Simba wamecheza Kaitaba wamefungwa mbili na kushinda moja.
Msimu wa 2016-17, Aprili 2 Kagera Sugar waliifunga Simba mabao 2-1; ule wa 2017-18 Simba walishinda mabao 2-0 wakati msimu uliopita Kagera waliendeleza ubabe nyumbani kwa kuwatungua Simba mabao 2-1.
Simba mara baada ya kumaliza na Kagera Sugar ambao msimu uliopita licha ya kuchukua ubingwa lakini walifungwa mechi zote mbili za nyumbani na ugenini, Oktoba 23 watacheza na Azam FC kwenye Uwanja wa Taifa.
Rekodi zinaonyesha Simba na Azam katika mechi nne zilizopita walipokipiga Uwanja wa Taifa, Wekundu wa Msimbazi walishinda mara mbili na kutoka suluhu mbili. Msimu wa 2017-18, mechi ya mzunguko wa kwanza iliisha kwa suluhu wakati ya mzunguko wa pili Simba walishinda bao 1-0, msimu uliopita katika mechi ya kwanza Mei 13 ilimalizika kwa suluhu na mzunguko wa pili ilimalizika kwa Simba kushinda mabao 3-1.
Simba wataendelea kubaki Dar es Salaam kucheza na KMC Oktoba 19 na rekodi zinaonyesha msimu uliopita ndio ulikuwa wa kwanza KMC kucheza Ligi Kuu Bara na walipokutana na Simba Uwanja wa Taifa walifungwa mabao 2-1 yaliyofungwa na Adam Salamba na Said Ndemla huku lao likifungwa na James Msuva.
Baada ya kumaliza mechi hizo mbili za Dar es Salaam, kikosi cha Simba kitasafiri hadi Mara ambako watamalizana na Biashara United ikiwa ni mwendo wa kilomita 1,370 kutoka Dar es Salaam. Mchezo huo utapigwa Novemba 7.
Msimu uliopita Biashara ndio ulikuwa wao wa kwanza kucheza Ligi Kuu ambapo wakiwa nyumbani Uwanja wa Karume mjini Musoma walipigwa mabao 2-0 kupitia kwa John Bocco.
Baada ya kutoka Mara, Simba watasafiri umbali wa kilomita 674 hadi mkoani Singida ambapo Novemba 11 watacheza na Singida United wakiwa nyumbani Namfua. Simba imeshinda mechi zote mbili katika dimba hilo.
Singida United walipanda Ligi Kuu Bara msimu 2017-18 na kwenye mechi zote dhidi ya Simba walichezea kichapo. Kwanza walifungwa bao 1-0 na msimu uliopita walifungwa tena 2-0.
Baada ya kumalizana na Singida United kikosi hicho cha Simba kitarejea Dar es Salaam umbali wa kilomita 696 kuendelea na harakati zingine.
Kama itashinda mechi hizo tano itavuna alama 15 ambazo zitaendelea kuwaweka kileleni mwa msimamo kwani watakuwa na jumla ya pointi 18 ambazo zitawaweka pazuri.

KOCHA SIMBA
Kocha wa Simba, Patrick Aussems anasema baada ya kupata matokeo ya kuumiza katika Ligi ya Mabingwa Afrika na kutupwa nje ya mashindano wamehamishia nguvu katika Ligi Kuu Bara ili kupata matokeo mazuri mfululizo. Aussems anasema kila timu inatamani kuifunga Simba na wao wanafahamu hilo, lakini wamejipanga kushinda kila mchezo ili kurejea kwenye mashindano ya kimataifa msimu ujao pamoja na kutetea ubingwa.
“Ndio maana wakati huu ligi imesimama kupisha timu za taifa tunaendelea na maandalizi,” anasema kocha huyo.
“Hii ni kuandaa kikosi kuwa katika hali ya ushindani na kupata matokeo mazuri. Tunahitaji kupunguza presha mapema katika kuvuna pointi ili tunapofika mwishoni tuwe kwenye nafasi nzuri bila ushindani.”

KIKOSI CHA SIMBA
Aliyekuwa kocha wa timu ya taifa ya vijana chini ya miaka 17, Oscar Milambo anasema kikosi cha Simba kimefanya usajili mzuri na kushindwa kufanya vizuri katika mashindano ya kimataifa, lakini wanaweza kuwa bora katika mashindano ya ndani.
“Wanaweza kutetea ubingwa lakini kwa muda niliopita kuiona timu yao ikicheza mechi kuna wachezaji wapya wazuri ambao wakiunganisha nguvu na wale ambao walikuwa kwenye timu msimu uliopita wanaweza kutetea mataji,” anasema Milambo.

MABOSI MSIMBAZI
Mwenyekiti wa klabu ya Simba, Swedy Mkwabi anasema uongozi wao unaendelea kufanya kila  wanaloweza ili kuhakikisha katika mashindano yote ya ndani wafanye vizuri na sio kujitokeza tena yale yaliyowakuta katika mashindano ya kimataifa.
Mkwabi anasema kikosi chao ni kizuri kutokana na usajili ambao wameufanya sambamba na wachezaji waliokuwa kwenye timu msimu uliopita huku wakihamishia nguvu kutetea taji lao.
“Haikuwa malengo yetu kuondolewa mwanzoni kimataifa, lakini ndio imeshatokea, hatutachoka kujaribu tena. Kwa maana hiyo ili kurudi huko ni kufanya vizuri kwenye ligi na kuchukua ubingwa tena, jambo ambalo kwetu linawezekana,” anasema Mkwabi.