Wachezaji Taifa Stars wajazwa noti, Burundi hawatoki Uwanja wa Taifa

Muktasari:

Stars ililazimisha sare ya 1-1 katika mechi yao ya awali ugenini Burundi na sasa wanahitaji matokeo ya 0-0 ama ushindi wowote ili kuingia hatua ya makundi. Viingilio ni Sh 2,000 kwa mzunguko na Sh 5,000 kwa VIP B na C.

Dar es Salaam. Shirikisho la Soka nchini (TFF), limewatengenezea mazingira mazuri wachezaji wa Taifa Stars iliwaweze kupata matokeo chanya katika mechi yao ya marudiano ya kuwania kufuzu kwa fainali za Kombe la Dunia  2022 dhidi ya Burundi leo.
Stars ililazimisha sare ya 1-1 katika mechi yao ya awali ugenini Burundi na sasa wanahitaji matokeo ya 0-0 ama ushindi wowote ili kuingia hatua ya makundi.
Katibu Mkuu wa TFF, Wilfred Kidao alisema: “Upande wa posho tumewaongezea kwa kiwango kikubwa sana tofauti na posho iliyokuwa inatolewa huko nyuma, siwezi kusema kwa kiwango gani, lakini posho yao hivi sasa ni nzuri, hoteli wanazokaa ni tofauti na za kipindi cha nyuma na hii yote tunawafanya waone kweli wapo katika timu ya Taifa.”
Akizungumzia mchezo huo, alisema kwa maandalizi waliyofanya wana kila sababu ya kusonga mbele.
“Tunataka kwenda katika Kombe la Dunia lakini lazima tuanzie kwenye kuitoa Burundi, tukifanikiwa kuitoa tutaingia kwenye hatua ya makundi sehemu ambayo itakuwa sio ngumu sana kwetu kwani tukipata sare za ugenini na tukihakikisha tunashinda mechi zetu za nyumbani kila kitu kinawezekana kusonga mbele,” alisema.
Aliongeza jambo la msingi linalotakiwa kuangaliwa hivi sasa ni umoja kuelekea katika mchezo huo na kuachana na makundi ambayo yanataka kuanzishwa kwa kipindi hiki.
“Hii ni timu yetu sote, kwahiyo tumalize hili jambo kwanza na mengine ndio yatafuata, yapo makundi mengi ya uhamasishaji, lakini tukimaliza hili tutakaa na kujua tunasogea vipi mbele,” alisema.
Awatuliza Watanzania
Katika mchezo wa kwanza uliochezwa ugenini, baadhi ya viongozi na Watanzania waliokuwa katika msafara walifanyiwa vurugu na mashabiki wa Burundi na timu ilishindwa kuingia katika vyumba vya kuvalia wakati wa mapumziko kutokana na vurugu hizo.
Lakini Kidao amewaomba Watanzania wasilipize kisasi na walichukulie suala hilo kama changamoto nyingine.
“Niliongea na Katibu Mkuu wa Chama cha Soka Burundi na nilimuhakikishia awe na amani, timu yake haitafanyiwa vurugu, nawaomba Watanzania wala wasiwe na mawazo ya kufanya vurugu kwasababu sisi tunaaminika kwa nidhamu na ukarimu tulionao,” alisema.
Aliyekuwa Katibu Mkuu wa Shirikisho la Mpira wa Miguu nchini, Angetile Osiah alisema uwepo wake katika kamati ndogo ya uhamishaji kwa Stars ni kuhakikisha timu hiyo inasonga mbele dhidi ya Burundi.
Akizungumza na waandishi wa habari, Angetile alisema wachezaji wamekuwa wa kwanza kuonyesha uzalendo kwa kujituma muda wote.
“Ukiangalia namna ambavyo wamecheza katika mchezo wa kwanza wanaonyesha dhahiri ni wazalendo, hata goli ambalo limepatikana unaona Samatta alihakikisha mpira mpaka unaingia ndani ya nyavu,” alisema.
Samatta alimkinga beki wa Burundi ambaye alikuwa anajiandaa kuokoa juu ya mstari wa lango mpira uliopigwa na Saimon Msuva na kuhakikisha unaingia wavuni.
Viingilio ni Sh 2,000 kwa mzunguko na Sh 5,000 kwa VIP B na C.