Ligi Kuu Bara yalamba udhamini wa Sh420Mil wa KCB Benki

Wednesday September 4 2019

Ligi Kuu Tanzania Bara, Mwanaspoti, yalamba udhamini, wa Sh420Mil wa KCB Benki

 

By Majuto Omary

Dar es Salaam. Benki ya KCB Tanzania imengia mkataba wa Sh420 milioni kudhamini Ligi Kuu ya Tanzania Bara.

Huu ni msimu wa tatu kwa benki hiyo kudhamini Ligi Kuu ya Tanzania Bara ambapo mara ya kwanza ilikuwa msimu wa 2017/18 kwa kutoa Sh325 milioni na msimu uliopita ilitoa Sh420 milioni vile vile.

Mpaka sasa benki ya KCB imetumia kiasi cha Sh1.165 bilioni za kitanzania kwa ajili ya kudhamini Ligi Kuu ya Tanzania Bara.

 Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya KCB, Cosmas Kimario alisema kuwa pamoja na dhamira ya benki hiyo kurudisha kwa jamii, udhamini huo pia ni fursa kubwa kwa benki ni kuchangia maendeleo ya soka na kukuza vipaji kwa wachezaji.

Kimario alisema kuwa mpira wa miguu unatengeneza ajira kwa vijana na kupunguza makali kwa timu zinazoshiriki katika ligihiyo yenye jumla ya timu 20.

“Matarajio ya benki yetu ni kuona wachezaji wa Tanzania wanafanya mazoezi kwa bidii na kuzipigania timu zao ili kuweza kushinda zawadi nono za ligi ambazo zitatolewa na wadhamini wengine, tunajisikia fahari kuunga mkono maendeleo ya soka nchini,” alisema Kimario.

Advertisement

“Sisi Benki ya KCB, mbali na biashara tunatimiza wajibu wetu katika jamii inayotuzunguka kwa kuiunga mkono serikali yetu kupinga umasikini nchini. Hivyo pia tunasaidia jamii hitaji kupitia sekta za: elimu, afya, mazingira, wajasiriamali, watoto waishio katika mazingira magumu,” alisema.

Rais wa TFF, Wallace Karia aliishukuru Benki ya KCB Tanzania kwa kuidhamini Ligi kuu Tanzania Bara na udhamini huo utasaidia kufanikisha msimu huu wa ligi kuu 2019/20.

Karia alisema kuwa theluthi mbili ya fedha hiyo itakwenda moja kwa moja kwa vilabu kwa mujibu wa utaratibu wao.

“Siwezi kusema kila timu itapewa kiasi gani cha fedha, hata wakati wa kutangaza udhamini wa Vodacom Tanzania, nilisema kuwa thleuthi mbili zitagawiwa kwa timu ambazo zipo ishiriki, ni vigumu kwa sasa kusema timu zinapewa kiasi gani cha fedha,” alisema Karia.

Hafla ya kutia saini makubaliano hayo imehudhuriwa na Mwenyekiti wa Bodi ya Benki ya KCB Tanzania, John Ulanga, Katibu Mkuu TFF,. Kidao Wilfred, Mwenyekiti wa bodi ya Ligi Kuu, Steven Mnguto na Afisa Mtendaji Mkuu wa Bodi ya Ligi, Boniface Wambura.

Advertisement