Van Dijk apewa tena Ronaldo, Messi tuzo Fifa

Muktasari:

Beki huyo wa Liverpool, Mdachi Van Dijk aliwabwaga wakali hao kwenye tuzo za kumsaka mchezaji bora wa mwaka wa Ligi ya Mabingwa Ulaya, lakini sasa atakabiliana nao tena katika tuzo ya Fifa kwa upande wa wachezaji wa kiume.

MILAN, ITALIA. KIMENUKA tena. Beki wa kati, Virgil van Dijk amepewa wapinzani walewale Lionel Messi na Cristiano Ronaldo kwenye kinyang'anyiro cha kumsaka mchezaji bora wa mwaka wa Fifa.
Beki huyo wa Liverpool, Mdachi Van Dijk aliwabwaga wakali hao kwenye tuzo za kumsaka mchezaji bora wa mwaka wa Ligi ya Mabingwa Ulaya, lakini sasa atakabiliana nao tena katika tuzo ya Fifa kwa upande wa wachezaji wa kiume.
Kiwango bora cha Liverpool kwa mwaka huu kimemfanya kocha wao, Jurgen Klopp naye kuingia kwenye mchakamchaka wa kuwania tuzo ya kocha bora wa mwaka sambamba na Pep Guardiola na Mauricio Pochettino, ambao wote amekuwa akichuana nao kwenye Ligi Kuu England.
Kipa wa Liverpool, Alisson atachuana na yule wa Manchester City, Ederson na wa Barcelona, Marc-Andre ter Stegen katika tuzo ya kipa bora wa mwaka, huku Messi akitajwa kwenye kinyang'anyiro cha tuzo mbili, ikiwamo ile ya Puskas inayohusiana na bao bora la mwaka ambapo atachuana na Juan Fernando Quintero na Daniel Zsori.
Beki Van Dijk anatarajia kwenda kuweka historia akibeba tuzo hiyo tena itakayotolewa baadaye mwezi huu huko Milan, Italia. Beki huyo alikuwa bora huko Liverpool na kuisaidia kushinda ubingwa wa Ligi ya Mabingwa Ulaya msimu uliopita.