Birigimana, Kalengo ni muda tu watakuwa sawa Yanga

Muktasari:

Kalengo aliyenaswa kutokea Zesco United ya Zambia anayecheza nafasi ya mshambuliaji wa kati, amejikuta akiwa kwenye wakati mgumu wa kucheza mbele ya washambuliaji Juma Balinya, David Molinga na Sadney Urikhobi.

Dar es Salaam. ISSAH Bigirimana na Maybin Kalengo wamekuwa hawana nafasi kwenye kikosi cha kwanza cha Yanga licha ya matumaini makubwa ambayo wengi walikuwa nayo juu yao wakati wanasajiliwa.
Lakini nyota hao wawili wamejikuta hawapati muda wa kutosha wa kucheza ndani ya kikosi hicho jambo ambalo limeanza kuleta hofu kuwa huenda viwango vyao viko chini.
Kalengo aliyenaswa kutokea Zesco United ya Zambia anayecheza nafasi ya mshambuliaji wa kati, amejikuta akiwa kwenye wakati mgumu wa kucheza mbele ya washambuliaji Juma Balinya, David Molinga na Sadney Urikhobi.
Mchezaji huyo mwenye umri wa miaka 20, katika mechi tano za hivi karibuni ambazo Yanga imecheza dhidi ya timu za Malindi, Township Rollers, Polisi Tanzania, AFC Leopards na Ruvu Shooting amecheza kwa dakika 163 tu kati ya 450 tena katika mechi tatu ambazo ni dhidi ya Ruvu Shooting aliyoingia kipindi cha pili dakika ya 63, ile ya kirafiki dhidi ya Polisi Tanzania aliyocheza kwa dakika zote 90 na mechi ya kirafiki waliyocheza na Malindi ambayo alipewa dakika 46.
Kwa upande wa Bigirimana (23), aliyenaswa kutokea APR amejikuta akiwa kwenye wakati mgumu wa kupata nafasi mbele ya Patrick Sibomana, Mapinduzi Balama na Mrisho Ngassa.
Kwenye mechi tano ambazo Yanga imecheza hivi karibuni, Bigirimana amecheza dakika 103 tu ambazo zote aliingia akitokea benchi katika mechi dhidi ya Malindi, Polisi Tanzania na AFC Leopards.

MSIKIE ZAHERA
Lakini kocha wa Yanga, Mwinyi Zahera anachukulia kitendo cha nyota hao kusotea benchi kwa mtazamo chanya na bado ana imani kubwa juu yao. Na kwa kudhihirisha hilo, Zahera amefichua sababu hasa iliyosababisha nyota hao wasipate nafasi ya kutosha kwa sasa.
“Bigirimana (anacheka kidogo) wakati timu ipo kwenye mazoezi makali Morogoro nimeambiwa aliwahi kuuliza mbona huku kuna mazoezi makali sana? Kule kwao timu nyingi hazina mazoezi ya nguvu kama huku,” alisema Zahera.
“Tulipokuwa tunataka kumsajili tuliangalia ufanisi wake uwanjani katika mechi, kuzoea hapa anahitaji muda, namuona ameanza kubadilika, mkumbuke pia aliumia nyama hivi karibuni.
“Kalengo naye licha ya kuwahi lakini apofika akawa na majeraha ya mguu wake, akakaa nje kwa muda mrefu, sasa naye ameanza kurejea anahitaji muda kukaa sawa.”
Zahera alitamba kuwa siku chache zijazo, nyota hao watakuwa moto wa kuotea mbali na kuisaidia Yanga kama ambavyo ana imani juu ya mshambuliaji David Molinga ‘Ndama’ ambaye amedai walinzi wa timu pinzani wajipange vilivyo kumkabili pindi akiwa fiti zaidi. “Kwa sasa amebakiza kufunga tu, najua hicho ndicho watu wanataka, namjua anajua kufunga lakini hataweza kufunga akikaa benchi anahitaji kuzoeana na wenzake. Alipocheza na Ruvu amecheza mechi ya kwanza subirini kama baada ya mechi nne mpaka tano mtamjua,” alisema Zahera.