Kikosi cha wa kimataifa Taifa Stars kinaiva

Muktasari:

Tathmini iliyofanywa imebaini kwamba licha ya kikosi cha Stars kwa sasa kuundwa na wachezaji mchanganyiko, bado imekuwa na uwezekano wa kikosi chake cha kwanza kuwa na wachezaji 11 ambao wote wanacheza soka la kulipwa nje ya nchi.

Dar es Salaam. Kuongezeka kwa idadi ya wachezaji wa Kitanzania wanaocheza soka la kulipwa nje ya nchi, huenda kukaifanya kikosi chake cha kwanza kutokuwa na mchezaji hata mmoja anayecheza ligi ya ndani miaka michache ijayo.
Tathmini iliyofanywa imebaini kwamba licha ya kikosi cha Stars kwa sasa kuundwa na wachezaji mchanganyiko, bado imekuwa na uwezekano wa kikosi chake cha kwanza kuwa na wachezaji 11 ambao wote wanacheza soka la kulipwa nje ya nchi.
Ingawa baadhi hawajapata fursa ya kuitwa kikosini, kikosi cha kwanza cha Stars chenye nyota wa kigeni kinaweza kuundwa na wachezaji David Kisu, Hassan Kessy, Nickson Kibabage, Abdallah Shaibu, Abdi Banda, Ally Ng’anzi, Saimon Msuva, Yahya Alghassan, Mbwana Samatta, Eliud Ambokile na Yahya Zaydi.
Kipa Kisu ambaye aliwahi kuzichezea Njombe Mji na Singida United, kwa sasa anafanya vizuri kwenye kikosi cha Gor Mahia ya Kenya na amedaka mechi mbili za hatua ya awali ya Ligi ya Mabingwa Afrika ambayo timu yake iliing’oa Aigle Noir ya Burundi kwa 5-1.
Kiwango bora cha Kisu kimefanya kipa aliyekuwa chaguo la kwanza wa Gor Mahia, Boniface Oluoch kusotea benchi.
Upande wa kulia anaweza kutumika Hassan Kessy wa Nkana FC ya Zambia ambaye hata kwenye Fainali za Mataifa ya Afrika (Afcon) zilizofanyika Misri mwaka huu alikuwa chaguo la kwanza kwa upande huu.
Aliyekuwa nyota wa timu ya Taifa ya vijana U-17 ‘Serengeti Boys’ iliyoshiriki Fainali za Afrika kwa vijana wa umri huo nchini Gabon 2017, Nickson Kibabage ambaye kwa sasa anacheza soka nchini Morocco kwenye kikosi cha Difaa el Jadida, anaweza kusimama beki ya kushoto.
Beki ya kati wapo Abdi Banda anayecheza soka la kulipwa Afrika Kusini kwenye kikosi cha Highland Parks kinachoshiriki Ligi Kuu nchini humo pamoja na Abdallah Shaibu ‘Ninja’ anayechezea LA Galaxy ya Marekani.
Mwingine anayecheza soka la kulipwa nchini Marekani katika klabu ya Minnesota, Ally Ng’anzi anaweza kucheza kiungo namba sita. Wingi ya kulia Msuva (Difaa el Jadida), namba nane Maka Edward anayecheza pia nchini Morocco kwenye klabu ya FC Tetoun. Straika namba 9, Mbwana Samatta wa KRC Genk ya Ubelgiji, Adi Yusuph aliyepo Blackpool inayoshiriki Ligi Daraja la Pili nchini England anaweza kupangwa sambamba na Samatta katika nafasi ya ushambuliaji na Yahya Alghassani anayecheza Al Wahda ya Falme za Kiarabu.
Kwenye benchi kunaweza kuwepo Eliud Ambokile (TP Mazembe), Eliuter Mpepo (Buildcon), Haji Mnoga (Portsmouth), Thomas Ulimwengu (JS Saoura) na Dickson Ambundo (Gor Mahia)