Dili la Sanchez kuondoka Manchester United pasua kichwa

Muktasari:

Inter Milan matumaini yake ni kumtangaza Sanchez kuwa mchezaji wao kabla hawajakipiga na Lecce, ambapo hiyo itakuwa mechi ya kwanza kwa kocha Antonio Conte nyumbani uwanjani San Siro tangu achukue mikoba ya kuinoa timu hiyo.

MANCHESTER, ENGLAND. MANCHESTER United itampiga chini Alexis Sanchez wiki hii, lakini jambo hilo linaweza kuwagharimu Pauni 13 milioni.
Man United wapo kwenye hatua za mwisho kabisa za kumfungulia mlango wa kutokea Sanchez akakipige kwa mkopo huko Inter Milan baada ya klabu hiyo ya Serie A kukubali kulipa nusu ya mshahara wa mchezaji huyo, Pauni 500,000 kwa wiki.
Hiyo ina maana kwamba Man United watakuwa wanaendelea kulipa nusu nyingine ya mishahara kwa kipindi chote cha msimu. Man United pia wanataka kufungulia mlango ya kuifanya Inter Milan kumbeba jumla Sanchez kwa ada ya Pauni 20 milioni itakapofika mwakani.
Lakini, Inter na Man United bado hawajafikia makubaliano ya kuhusu malipo ya Pauni 52 milioni ya kuhusu malipo yake kwenye mkataba wake kuanzia mwaka 2020. Mazungumzo ya jambo hilo yataendelea leo Jumatatu.
Inter Milan matumaini yake ni kumtangaza Sanchez kuwa mchezaji wao kabla hawajakipiga na Lecce, ambapo hiyo itakuwa mechi ya kwanza kwa kocha Antonio Conte nyumbani uwanjani San Siro tangu achukue mikoba ya kuinoa timu hiyo.
Conte amewataka mabosi wake kukamilisha dili la Sanchez kwa wakati baada ya kufanikiwa kumsajili Romelu Lukaku kutoka kwenye klabu hiyo ya Man United kwa ada ya Pauni 73 milioni.
Kocha wa Man United, Ole Gunnar Solskjaer alimwambia makamu mwenyekiti wa klabu hiyo, Ed Woodward kumuuza Lukaku baada ya straika huyo Mbelgiji kutoonekana mazoezini kwa siku mbili wakati kikosi kikiwa kwenye mazoezi ya kujiandaa na msimu mpya. Solskjaer pia amemwambia Sanchez, ambaye amekuwa kwenye kipindi kigumu kwa mwaka mmoja na nusu aliyokuwa Old Trafford, kwamba hatakuwa na uhakika wa kupata nafasi katika msimu huu.
Taarifa nyingine zinadai kwamba Man United itaingia gharama ya kumlipa Pauni 22 milioni kwa mwaka Sanchez kwa dili hilo la kwenda Inter Milan. Hiyo ni kwa sababu Inter wao wapo tayari kuchangia Pauni 80,000 tu kwa wiki kwenye mshahara wa mchezaji huyo, kutoka kwenye mkwanja wa Pauni 505,000 kwa wiki, hapo itakuwa imebaki Pauni 425,000 kwa wiki, ambayo Man United watalazimika kulipa, kiwango kitakachofanya ifikie Pauni 22 milioni kwa mwaka.