Pepe aivunja rekodi ya mechi 50 kutopitika kwa beki Van Dijk

Muktasari:

Ni hivi, beki huyo wa Liverpool, Van Dijk alikuwa akishikilia rekodi matata kabisa kwenye Ligi Kuu England kwamba hakuna mchezaji aliyewahi kumpita na mpira mbele yake tangu Machi 2018, zikipita mechi 50 za ligi hapo katikati.

LIVERPOOL, ENGLAND. HATIMAYE, rekodi ya Virgil van Dijk ya kuwa beki kisiki asiyepitika kwenye Ligi Kuu England imevunja na staa mpya wa Arsenal, Nicolas Pepe.
Ni hivi, beki huyo wa Liverpool, Van Dijk alikuwa akishikilia rekodi matata kabisa kwenye Ligi Kuu England kwamba hakuna mchezaji aliyewahi kumpita na mpira mbele yake tangu Machi 2018, zikipita mechi 50 za ligi hapo katikati.
Lakini, Jumamosi huko Anfield kwenye mechi dhidi ya Arsenal, Mdachi huyo alikutana na kiboko yake, Pepe alipopita na mpira mbele ya beki huyo kisiki. Hata hivyo, mechi hiyo ilimalizika kwa Liverpool kuwachapa Arsenal 3-1.
Van Dijk ni beki ghali kwenye kikosi cha Liverpool, akisajiliwa kwa Pauni 75 milioni kutoka Southampton, Januari 2018, huku winga Nicolas Pepe akiwa mchezaji ghali huko Arsenal, ambapo amenaswa kwa mkwanja wa Pauni 72 milioni akitokea Lille.
Mashabiki wa Arsenal wala hawakujali kuhusu kupoteza mechi na kufurahia kwa namna ambavyo staa wao mpya alimtesa beki anayeonekana kuwa bora zaidi katika Ligi Kuu England.
Shabiki mmoja alindika kwenye Twitter: "Pepe alimfanya Van Dijk kama mdoli. Ni Henry mpya."
Huku mwingine, aliandika: "Imemchukua dakika tano tu, Pepe kupita na mpira mbele ya beki Van Dijk."
Shabiki aliyetambulika kwa jina la 3xceptional aliandika: "Pepe amepita na mpira mbele ya Van Dijk kwa mara ya kwanza kuliko wachezaji katika mechi nyingi, hii ni hatari."
Mashabiki wa Liverpool walijibu, ambapo mmoja aliandika: "Naona mashabiki wa upinzani wanafurahia Pepe kupita na mpira mbele ya Van Dijk."
Mwingine aliandika: "Hii inaonyesha jinsi gani Van Dijk alivyobora, maana watu wanashangilia utadhani wamefunga bao vile."