No Agenda: Diamond ameshakuwa baba, atulie watoto wampe wajukuu

Muktasari:

Ukiambiwa mauzo ni kiwango cha diamond, ujue hapo ni zaidi ya platinum 10, kwani platinum moja ni mauzo nakala milioni moja. Ni gold 20, maana gold moja ni nakala laki tano

FEBRUARI 2014, 50 Cent, alipokuwa anasaini mkataba na kampuni ya usambazaji ya Caroline, inayomilikiwa na taasisi ya Universal Music Group (UMG), alisema, alikuwa bado anadaiwa albamu moja na lebo ‘joint’ ya Shady-Aftermath, lakini alikubaliana kiroho safi na Dre pamoja na Eminem.
50 alisema: “Mimi ni kesi na mazingira maalumu. Ni kwa sababu nina uhusiano imara na Eminem pamoja na Dre. Hawataki nisiwe na furaha. Wanathamini urafiki wetu kwa namna ambayo hawataki kuuhatarisha kwa sababu ya pesa.”
Eminem na Dre ni kina nani? Tuanze na Eminem! Rejea miaka ya 1990, Eminem akiwa janki anayetokea mitaa ya mateja wa cocaine na heroin, Detroit, Marekani, mboni za macho yake hazikuona nuru, jicho halikufumbuka kuona mafanikio.
Tiba ya Eminem ikawa kusikiliza ngoma za jasusi wa lyrics za Hip Hop, Tupac Shakur. Mashairi ya Tupac yakamfanya aamini “kesho” ni laini na tamu, akavumilia magumu ya “leo” kwa matumaini.
Rejea miaka 20 iliyopita, Eminem alipokutana na Dre, ilikuwa mwaka 1999. Dre akamsaini Eminem kwenye kampuni yake ya Aftermath Entertainment. Kabla ya hapo, Eminem mwaka 1996, alitoa albamu ya kwanza, Infinite, ambayo ilichezea mabao mengi sokoni. Kwa kifupi, Infinite ilimpa za uso Eminem, ikamfanya ayaone maisha ya muziki ni magumu.
Akabaki na imani, mashairi ya Tupac yakamwambia japo anaona giza, taa itawaka, mbele ni ukuta, hakuna pa kupita, atatoboa na kupita hapohapo ukutani. Mwaka 1997, alitoa EP (extended play), yaani albamu ndogo, Slim Shady EP, ikala kitofa cha kichwa!
Albamu ya pili ya Eminem, The Slim Shady LP, ndio mzigo wa kwanza ‘uliofanywa’ na babu kichaa wa midundo, Dre. Mauzo yake yakawa ni usiniambie. Nakala milioni 5 zikauzika. Ikafuata albamu ya tatu na nne, The Marshall Mathers LP (2000) na The Eminem Show (2002), zote zilikufuru mauzo kwa kiwango cha diamond, yaani nakala zaidi ya milioni ziliuzika kwa kila moja.
Ukiambiwa mauzo ni kiwango cha diamond, ujue hapo ni zaidi ya platinum 10, kwani platinum moja ni mauzo nakala milioni moja. Ni gold 20, maana gold moja ni nakala laki tano. Hivyo, kufikia mwaka 2002, Eminem alishaukwaa na utajiri mkubwa.
Tusifike kwenye mafanikio makubwa ya albamu ya tano ya Eminem, Encore ya mwaka 2004 na nyingine zilizofuata, zilizomshusha Tupac kama mwana-Hip Hop namba moja kwa mauzo, kisha akaa yeye (Eminem), shikilia hapo kuwa mwaka 2002, Eminem alishakuwa tajiri!
Sasa tukubaliane, Dre ni baba wa kimuziki wa Eminem. Hilo Eminem huwa hafichi. Hutamka kuwa Dre aliokoa maisha yake, bila kumsaini kwenye lebo ya Aftermath, angeweza kufa, kujiua au kutopea kwenye vitendo ambavyo vingemwingiza kwenye giza totoro la kimaisha!
Turejee pale mwaka 2002 Eminem tayari alishakuwa tajiri. Eminem alianzisha lebo yake, Shady Records. Mwaka huohuo 2002, Eminem alipokea mixtape CD ya 50, “Guess Who’s Back” kutoka kwa wakili wa 50, aliyekuwa akifanya kazi na meneja wa Eminem, Paul Rosenberg.
50 wakati huo alikuwa ametoka kutobolewa matundu tisa ya risasi, katika shambulio la kuchomoa uhai wake. Eminem akavutiwa na 50. Akampeleka LA (West Coast), yalipo makao makuu ya Aftermath. Eminem akamtambulisha 50 kwa Dre. Wakamsaini.
Lebo ya Eminem, Shady Records na Aftermath ya Dre, zikaunda ushirika wa pamoja (joint venture), wakauita Shady-Aftermath, wakafyatua albamu ya kwanza ya 50, Get Rich  or Die Tryin’ (2003), ikafuata The Massacre (2005), Curtis (2007), Before I Self Destruct (2009).
Albamu ya tano, Animal Ambition, 50 aliitoa chini ya lebo yake ya G-Unit na kusambazwa na kampuni ya Caroline. G-Unit ni lebo ambayo 50 aliianzisha mwaka 2003, baada ya mafanikio makubwa ya albamu yake ya Get Rich or Die Tryin’. Waliosainiwa G-Unit ni Lloyd Banks, Tony Yayo, Young Buck, The Game na Olivia.
Sasa tunene lugha ya mataifa; Eminem baada ya kukua kimuziki, alianzisha mji wake, Shady, akampata mtoto ambaye ni 50. Hivyo, 50 ni mjukuu wa Dre. Ni kama ambavyo Dre alipokuwa Deathrow ya Suge Knight, alipojiona amekua, alianzisha mji wake, Aftermath mwaka 1996.
50 alipojiona amekua, akachukua kundi lake la G-Unit na kulifanya kuwa kampuni ya kibiashara. Hivyo, kina Banks, Yayo na Olivia ni wana kwenye muziki kwa 50, hivyo ni wajukuu wa Eminem. Ni watukuu wa Dre.
Huo ndio mwendo. Ni fahari kwa baba kupata watoto, nao watoto wakikua, ni fahari kukupa wajukuu. P Diddy alipokuwa anachokonoa njia ya mafanikio, alianzia Uptown Records kwa Andre Harrell mwaka 1990. Alipotoka Uptown alianzisha Bad Boy Entertainment. Hivyo, Harrell ni baba wa Diddy kama ambavyo Diddy ni baba wa akina Craig Mack, Notorious BIG, Mase na wengine.
Imenipendeza mimi binafsi, kupitia utawala wa dola ya jamhuri ya ubongo wangu, kufanya marejeo yote hayo kutoka kwa Dre, Eminem, 50 na G-Unit mpaka Harrell, P Diddy na Bad Boy, ili niwafikie Diamond Platnumz na WCB, mpaka Harmonize na Konde Gang.
Diamond alizaliwa kimuziki pale Sharobaro Records kwa Bob Junior. Hivyo, Diamond ni mtoto wa Bob Junior. Diamond alipokua, hasa baada ya kushindana na baba yake, alianzisha mji wake, WCB, akapata watoto, Harmonize, Rich Mavoko, Lavalava na Mboso.
Aliwaasili watoto wawili, Queen Darleen na Rich Mavoko. Baadaye Mavoko akaanzisha lebo yake, Bilionea Kid na sasa mtoto mkubwa kumzaa mwenyewe, yaani Harmonize, tayari ameamua kutafuta mji wake, Konde Gang, bila shaka anaandaa mazingira ya kupata watoto ambao watakuwa wajukuu wa Diamond.
Hivyo, Harmonize kuondoka WCB ni fahari kubwa kwa Diamond kuona kuwa amekuza, amwache akajenge mji wake, amtakie mafanikio, angoje kuona wajukuu.
Baba mzuri hatapenda kuona wanaye wanazeekea nyumbani. Kama ulikua na ukajenga ngome yako, ukikataa mwanao naye ajenge ya kwake ni ubinafsi.
Diamond ampe mkono mwema Harmonize, maana ukikuza mtoto na kama hana matatizo lazima akuletee wajukuu. Sema amwambie kuwa kwenda na mabodyguard misibani sio hulka njema. Ni ushamba. Harmonize alizingua kuvamia na mabodyguard kwenye msiba wa Mbalamwezi wa kundi la The Mafik.