Yanga mpooo... Kisu kipya hicho Simba mwanangu

Monday August 19 2019

Yanga mpooo, Mwanaspoti, Tanzania, Kisu kipya hicho, Simba mwanangu

 

By THOBIAS SEBASTIAN

Dar es Salaam. HUKO kitaani kwa sasa mashabiki wa Simba wanasumbua sana. Kisa ni mziki mnene uliowashwa na nyota wao wapya. Kuanzia Francis Kahata, Shiboub Sharaf Eldin na winga Deo Kanda. Hapo ni mbali na Wabrazili wao watatu.
 Usajili wa nyota hao umeonekana ni shida na mateso makubwa kwa wale wa Yanga kwa namna Simba wanavyowatambia.
Lakini shida wanayotaka kuileta mabosi wapya wa Simba ndio balaa na kama mipango yao itaenda kama watakavyo, Yanga wajiandae mapema aisee.
Ipo hivi. Mabosi wa Simba walipata ugumu wa kukamilisha usajili wa nyota mmoja wa kigeni wakileta mshambuliaji wa kuziba nafasi ya Emmanuel Okwi.
Mabosi hao wakawa wanampigia hesabu straika wa Lusaka Dynamos, Chris Mugalu, lakini wakapata ugumu kwani jamaa alishasaini mkataba wa awali Zesco United iliyopo chini ya George Lwandamina. Wakaamua wakaushe, ili kusubiri dirisha dogo, lakini wiki iliyopita wakiwa Msumbiji wakati Simba ikivaana na UD Songo wakajikuta wakivurugwa kabisa kutokana na soka tamu alililopiga nahodha wa wenyeji wao, Luis  Miquissone.
Fasta kina Crescentius Magori na wenzake buana wakaitana chemba na kujadiliana kwa jina kisha kuamua kumfungia kazi, ili wamshushe Msimbazi kukinukisha na kina Kahata.
Kiungo huyo mshambuliaji anayemudu pia winga ya kushoto, mwenye uwezo wa kutumia miguu yote, lakini ule wa kushoto ndio anakuwa mtamu zaidi ana umri wa miaka 24 tu. Na hicho ndicho kilichowavuruga mabosi hao wa Msimbazi na kukubaliana kumvuta kwenye dirisha dogo kumaliza tatizo linalowasumbua safu ya mbele.
Shughuli ya winga huyo inajulikana vyema kwa mabeki walioanza katika mechi hiyo ya Msumbiji,Shomary Kapombe, Gadiel Michael, Pascal Wawa na Erasto Nyoni kwani muda mwingi aliwasumbua kwa chenga zake na kutengeneza nafasi kwa wenzake.
Mbali na usumbufu wake uwanjani, lakini Miquissone pia ni hodari wa kufunga, kiasi kina Kahata na Deo Kanda wanasubiri wake na hicho ndicho kilichowafanya mabosi wa Simba kumsaka wakitaka hata wamlete kwa mkopo kutoka timu yake itakayokuja nchini wiki hii.
Taarifa kutoka chanzo cha kuaminika Simba, ni kwamba baada ya mechi kumalizika mabosi wa Simba walioambatana na timu Msumbij waliongea na winga huyo sambamba na viongozi wake ili wamvuite dirisha dogo ili kuleta shida kwa wapinzani wao.
Chanzo hicho kinadokeza kuwa, Simba imejulishwa kuwa, winga huyo amemwaga wino wa miaka minne kuitumikia Mamelodi Sundowns ya Afrika Kusini na kuwepo kwake UD Songo ni kwa mkopo kitu ambacho hata wao wanaweza kumbeba kama wanamtaka.
“Kwa namna ya uchezaji wake na umri alionao, Simba imeapa kufanya kila njia kumvuta kwani inaamini ataisaidia, hata ukipitia clip za mechi zake za nyumba jamaa anaonekana ni mtu (fundi kwelikweli) buana,” chanzo hicho kilisema.
Mwanaspoti lilimsaka Ofisa Mtendaji Mkuu wa Simba, Crescentius Magori juu ya ukweli wa taarifa hizo naye alisema katika misimu ambayo wamefanya usajili makini basi ni huu na kwamba nyota huyo amewavutia kwa aina ya soka lake, japo bado ni mapema mno.
“Miquissone ni mchezaji mzuri hasa baada ya kumuona katika mechi ya kule Msumbuji na kama kutakuwa na mahitaji naye hilo linatakiwa kutoka katika benchi la ufundi, ingawa tunafahamu nyota huyo ana mkataba wa miaka minne na klabu moja kubwa ya Afrika Kusini kwa maana hiyo si jambo rahisi kumpata,” alisema Magori.
Magori alisisitiza ni kweli wanataka kuboresha safu ya ushambuliaji na wanawafuatilia wachezaji wengi wanaofanya vizuri katika eneo hilo katika ligi mbalimbali, lakini suala la nani aje Msimbazi linabaki kuwa maamuzi ya Kocha Patrick Aussems.
Mchezaji huyo aliyezaliwa Mei 25, 1995 katika Mji wa Tete, Msumbiji ana urefu wa Mita 1,70 akiwa anaichezea pia Timu ya Taifa ya Msumbiji na yupo chini ya uwakala wa Wimbi Foot inayowasimamia wachezaji kadhaa akiwamo ndugu yake na Haruna Niyonzima, aitwaye Ally Niyonzima wa Rwanda.

Advertisement