Adi Yussuf ni muda tu, vita ya namba Blackpool wala haimsumbui kichwa

Muktasari:

Adi anasema siku zote amekuwa akifurahia changamoto hivyo yupo tayari kukabiliana nazo ili kuwa sehemu ya mafanikio ya Blackpool ambayo ina malengo ya kurejea Ligi Kuu England.

MAMBO magumu. Ndo unavyoweza kusema kuhusu mshambuliaji wa kimataifa wa Tanzania anayekipiga katika klabu ya Blackpool inayoshiriki Ligi Daraja la Pili England (League One), Adi Yussuf.
Unaambiwa mambo si mambo kwake hadi sasa katika ligi hiyo ya tatu kwa ubora nchini huko kutokana na kutokupata nafasi ya kucheza mbele ya Armand Gnanduillet ambaye amekuwa akitumika kama mshambuliaji wa mwisho (namba tisa) kwenye kikosi hicho mara kwa mara tangu kuanza kwa msimu huu.
Hata hivyo, kutopata nafasi kwa Adi, mwenyewe anadai hakuchukulii kwa mtazamo hasi, bali ameona ni kama changamoto na kwa sasa ana kazi ya kufanya kuhakikisha anaingia kwenye mipango ya Kocha Simon Grayson.
Adi anasema siku zote amekuwa akifurahia changamoto hivyo yupo tayari kukabiliana nazo ili kuwa sehemu ya mafanikio ya Blackpool ambayo ina malengo ya kurejea Ligi Kuu England.
“Ushindani wa namba ni mkubwa, kila anayecheza kwenye nafasi ya ushambuliaji amekuwa akijituma ili kupata nafasi ya kucheza, tupo washambuliaji sita, hakuna ambaye anataka kukaa nje.
“Anayepata nafasi ya kucheza hayupo tayari kuchezea hiyo nafasi, uzuri kila mchezaji amekuwa akipewa nafasi ya kucheza kutokana na mwenendo wake mazoezini.
“Nimeikuta timu tayari ikiwa na wachezaji wa kikosi cha kwanza kwa hiyo isingekuwa rahisi nifike na kupata namba moja kwa moja, naamini nina uwezo wa kucheza lakini ni suala la muda,” anasema.
Mshambuliaji huyo msimu uliopita akiwa na Solihull Moors ya Daraja la Nne, aliifungia jumla ya mabao 14 ambayo yaliisaidia kumaliza nafasi za juu na kucheza Ligi ndogo ‘Playoff’ kuwania kupanda Daraja la Tatu.
Mara baada ya kupoteza nafasi ya kupanda daraja kabla ya hata kutua nchini kwa ajili ya kujiunga na timu ya taifa ya Tanzania ‘Taifa Stars’ kujiandaa na fainali za Mataifa ya Afrika (Afcon) zilizofanyika Misri, alijiunga na Blackpool kwa kusaini mkataba utakaomalizika 2021.
Adi anasema amekuwa na program zake binafsi ambazo anaamini zitamsaidia kwenye vita aliyonayo ya kuwania nafasi ya kucheza kikosi cha kwanza cha timu hiyo ambayo imeuanza vizuri msimu huu wa Daraja la Pili England.
“Bila ya juhudi binafsi ni ngumu kufikia lengo. Nimekuwa nikifanya mazoezi na marafiki zangu na hata pale inapobidi kufanya mwenyewe nimekuwa nikijitoa,” anasema.
Mbali na Adi kukabiliana na ushindani mkubwa wa namba kutoka kwa Gnanduillet  pia ana kibarua kizito mbele ya Nathan Delfouneso na Joseph Nuttall ambao kama Blackpool ikicheza  mfumo wa 4-3-3 basi nyota hao hucheza pamoja  kwenye safu ya ushambuliaji ya timu hiyo.
Adi ambaye anavalia jezi namba 19, alikuwa benchi kwenye mchezo uliopita wa kombe la Ligi dhidi ya Macclesfield Town ambao walitoka sare ya mabao 2-2 ndani ya dakika 90 kabla kuondolewa kwa mikwaju ya penalti 4-2.
Akiuzungumzia ushindani uliopo kwenye Ligi Daraja la Pili, Adi anasema ni mkubwa ukilinganisha na ule wa Daraja la Nne ambako alikuwa akicheza msimu uliopita wa 2018/19.
“Aina ya mpira wa England unafanana lakini ushindani unatofautina ndiyo maana huwa rahisi kwa timu za madaraja ya chini kuzipa changamoto timu za madaraja ya juu.
“Msimu uliopita wa Kombe la FA, nikiwa Solihull Moors, tuliwasumbua sana Blackpool na niliwafunga japo tulikuwa madaraja ya chini. Aina ya mpira wa nchi hii kufanana kulitufanya kuweza kumudu kushindani nao,” anasema.
Katika mchezo ambao Adi anauzungumzia, chama lake la zamani liliondolewa kwa jumla ya mabao 3-2, mchezo wa kwanza ambao walikuwa nyumbani walitoka suluhu na katika marudino walikubali kipigo cha mabao 3-2.
Mabao ya Solihull Moors kwenye mchezo huo, yalifungwa na Adi dakika ya 33 na 51 na ilikuwa kwa mkwaju wa penalti.
Adi alianza maisha yake ya soka kwenye klabu ya Leicester City ambayo inashiriki Ligi Kuu England kabla ya kwenda kwa mkopo Tamworth na baadae kusajiliwa na Burton Albion.
Mshambuliaji huyo ni kati ya wachezaji wa Kitanzania, ambao wamezichezea klabu nyingi zaidi, pia amezichezea, Lincoln City,