Unaambiwa Mkoba wa KMC Tanzania hajawahi kula umeme

Monday August 19 2019

Unaambiwa Mkoba wa KMC, Tanzania hajawahi, kula umeme, Mwanaspoti, Michezo, Mwanasport

 

By JUDITH FUMBO (TUDARCO)

NI aghalabu sana kwa mchezaji wa nafasi za ulinzi kucheza mfululizo au kumaliza soka lao bila kupewa kadi nyekundu.
Lakini sasa unaambiwa beki wa KMC aliyewahi kukipiga Mbao FC, Amos Charles ni mmoja ya wachezaji ambao kadi nyekundu wanazisikia na kuziona kwa wenzao, licha ya kucheza nafasi ambayo ni nadra kwa wachezaji wake kuepuka adhabu za namna hiyo. Nini siri ya mafanikio yake pamoja na mambo mengine katika maisha yake ya soka? Tiririka naye...!

AKILI NA NIDHAMU TU
Beki huyo wa kati anasema licha ya wakati mwingine kukutana na changamoto kubwa katika kujaribu kuwazuia washambuliaji wasumbufu, lakini amekuwa akifanya kazi yake kwa weledi na nidhamu ya hali ya juu ndicho kinachomsaidia asile umeme.
Anasema siku zote amekuwa akitumia akili na nidhamu kwa lengo la kujiweka salama na pia kuilinda timu yake isipate hasara pale atakapofanya makosa yanayomlazimisha kutolewa nje kwa kadi nyekundu. Hata kadi za njano anasema huwa anajitahidi kuziepuka kwani zikiwa nyingi nazo ni hasara kwa mchezaji na timu kwa ujumla.
“Sina rafu mbaya uwanjani nacheza mchezo wa kiungwana. Soka ni burudani, hivyo huwa naheshimu hilo, japo kwa kadi za njano sikumbuki idadi ya nilizoonyeshwa, lakini kwa nyekundu nashukuru nimekuwa nikishuhudia tu kwa wenzangu,” anasema.

MZUKA KWA MARCELO
Wachezaji wengi huchangua namba za mgongoni kutokana na sababu mbalimbali, na Amos anafichua siri kubwa kuhusu jezi yake.
“Navutiwa na uchezaji wa beki wa Real Madrid, Marcelo, ndiye aliyenifanya nikapenda kuvaa jezi namba 12 kama yeye, yote ni kutamani kufikia mafanikio kama aliyonayo ikiwa ni sambamba na kucheza soka la mafanikio kama yeye,” anasema.

JIKONI NAKO YUPO VIZURI
Ni nadra sana kuona kijana wa kiume ametoka katika majukumu magumu kama kucheza soka akaingia jikoni kupika. Wengi wao wamekuwa wakisingizia uchovu na kuamua kula hotelini ama kwenye vibanda vya ‘mama ntilie’ kwa wale ambao hawajaoa na walioona basi kazi yao ni kuwasumbua wake zao wawafanyie wepesi kwenye kuwaandalia chakula. Kwa Amos hilo ni tofauti.
Anasema yeye anapenda kula hivyo haoni tabu kuingia jikoni kuandaa msosi wake. Unaambiwa nyota huyo hataki chakula kikauke mdomoni kwani muda wote anapenda kujitafuna hasa akiwa nyumbani.
“Napenda kula wali maharage na mlenda ndio chakula changu bora, hasa nikitoka mazoezini kwasababu hulegeza misuli. Naweza pia kupika vyakula vya kurosti kama nyama, maini, kuku na wali,” anasema.

SOKA TU
Kila mwanadamu huwa na ndoto anazopigania kuzitimiza japo ni wachache sana ambao hufikia malengo.
Beki huyo wa KMC anabainisha kuwa yeye amefanikiwa kufikia ndoto yake kwani soka ndio kila kitu katika maisha yake hivyo hadhani kama ana ndoto nyingine. Analifanya soka kama maisha.
“Tangu nimegundua kuwa soka ndio kipaji changu nimekuwa nikizingatia zaidi huko tu, hata shule mimi nilikuwa nazingatia zaidi mchezo huo na ndio ulionipa umaarufu. Sifikirii kutoka huku na kufanya kitu kingine,” anasema.

NI ZAO LA MAKONGO
Makongo ni chuo cha soka hivyo ndio unaweza ukasema baada ya kubainika kuwa nyota wengi wanaofanya vizuri wametokea huko mfano ni kipa Beno Kakolanya wa Simba au Juma Kaseja wa KMC na wengie wengi.
“Nimeanza kucheza soka nikiwa na umri mdogo sana na ndio ilikuwa hulka yangu nilipoenda Makongo nilikutana na utamaduni wa kucheza mpira basi elimu sikuitilia maanani sana nikajikuta naingia moja kwa moja katika soka kitu ambacho naamini ndio kimenifanya nijulikane,”
“Ubora wangu katika sekta hiyo uliwavuta viongozi wa Yanga na kunichukua nicheze Yanga ya vijana ‘Yanga B’ ambayo pia sikudumu muda mrefu nilipandishwa ya wakubwa ambako sikufanikiwa kucheza mechi hata moja na kuamua kuondoka kwenda kutafuta changamoto kwenye timu nyingine,” anasema.
 “Niliondoka Yanga kwa sababu tangu niingie klabu hiyo sikufanikiwa kucheza hata mechi moja’’.alisema

YANGA YAMZINGUA
Wakati wachezaji wengi wa soka wanaocheza katika timu ndogo kama Mbao, Lipuli, Singida United wengio wao wanatamani kucheza Simba na Yanga basi unaambiwa Amos aliikimbia Yanga B aliyokuwa anaichezea na kwenda kujiunga Ruvu Shooting.
Anafunguka sababu za kutoka katika timu hiyo ambayo ni maarufu na imekuwa ikitoa wachezaji wengi ni kukosa nafasi ya kucheza wakati anaamini ana uwezo.
“Nilianza kucheza timu ya vijana lakini kutokana na uwezo wangu mkubwa wa kucheza nilipandishwa kikosi cha wakubwa lakini sikuwa na namba kikosi cha kwanza na hata kupata nafasi ya kucheza nikaamua kuondoka na kutimkia timu ambayo naweza kupata namba ya kucheza,” anasema.

TUKIO BAYA
Beki huyo anabainisha kuwa katika maisha yake hatakaa asahau tukio lililomuweka nje ya soka miezi sita.
“Nakumbuka nilikuwa nacheza nikapata tatizo la kuteguka goti ambalo lilinifanya nikae nje ya uwanja kwa muda wa miezi sita. Tukio hilo ndio baya sana kwangu kwani soka ndio linaendesha maisha yangu,” anasema.

RATIBA YAKE SASA
Beki Amos anabainisha kuwa akiamka kila siku asubuhi cha kwanza kwake ni kumuomba Mungu na baada ya hapo atachukua taulo kuingia bafuni kuoga kisha kuelekea mazoezini.
“Mazoezi huwa nafanya mara mbili nikiwa na timu, binafsi nafanya mara moja kwani ratiba huwa zinaingiliana hivyo nafuata ya mwalimu na baada ya hapo natenga muda wangu kidogo kwaajili ya mazoezi yangu mwenyewe,” anasema.

Advertisement