Presha Guardiola achanganyikiwa na VAR, adai inapendelea

Monday August 19 2019

Presha Guardiola, Tanzania, England, Mwanaspoti, achanganyikiwa na VAR, adai inapendelea, soka, EPL

 

Manchester, England. Kama kuna kitu kinamchanganya kwa sasa Pep Guardiola ni VAR. sio kama haipendi, hapana, anadai inachagua matukio. Anaishangaa na anaamini inatumika vibaya,
Juzi Jumamosi, kocha huyo wa Manchester City alishuhudia kwa mara nyingine VAR ikiinyima ushindi timu yake dhidi ya Tottenham baada ya bao la Gabriel Jesus kukataliwa katika dakika za majeruhi.
Bao hilo la dakika ya 92 ambalo lingekuwa la ushindi kwa City lilikataliwa kwa madai beki wa City, Aymeric Laporte aliunawa mpira kabla ya Jesus hajafunga. Na sasa Guardiola amedai VAR haikutumikia vema katika maeneo yote.
Kocha huyo ametoa mfano wa mpira ulioguswa na mkono na beki wa Chelsea, Andreas Christensen katika pambano la Super Cup dhidi ya Liverpool Jumatano iliyopita lakini mwamuzi hakutoa penalti. Lakini pia akaelezea bao lililokataliwa la Wolves dhidi ya Leicester City ingawa mazingira yalikuwa kama ya Christensen.
“Inabidi warekebishe. Matukio tofauti ndani ya uwanja hayapo wazi. Wakati Christinsen aliponawa haikuonekana kama amenawa leo Laporte anaonekana amenawa. Hilo ndilo ambalo inabidi tufafanue,” alisema kocha huyo.
Guardiola pia alikumbushia mpira ulioguswa kwa mkono na mshambuliaji wa zamani wa Tottenham, Fernando Llorente katika pambano la robo fainali Ligi ya Mabingwa wa Ulaya msimu uliopita lakini mwamuzi hakupiga filimbi.
“Kwanini haikupigwa filimbi wakati Llorente aliponawa msimu uliopita lakini leo imepigwa filimbi? Wakati mwingine wanaamini  mchezaji amegusa wakati mwingine hawaamini. Ilitokea wiki iliyopita kwa Wolves na tuliona kwa Chelsea Jumatano. Golikipa hakuwa katika mstari (Adrian) wakati penalti inapigwa,” alisema Guardiola.
Guardiola pia alilalamika VAR haikuwapa penalti wakati Erik Lamela alipomkaba shingoni kiungo wake, Rodri ndani ya boksi juzi kabla ya mapumziko.
“Ni penalti. Rodri alikwenda chini lakini wakati huo VAR ilikuwa inakunywa kahawa. Inabidi uone waziwazi. Lakini tuliona katika mechi, mtu mmoja ndio alifanya mawasiliano na waamuzi. Waombeni watu wa VAR, waombeni waje London. Mabosi wakubwa,” alisema Guardiola akiwataka wakubwa wa VAR watoe maelekezo England.
“Kilichotokea Ligi ya Mabingwa wa Ulaya msimu uliopita, bao la dakika za mwisho la Raheem ndicho ambacho kimetokea leo. Ni ngumu kukubali kwa sababu tunacheza vizuri na tunafunga bao zuri. Wao mara yao ya kwanza walipovuka nusu ya uwanja walifunga bao na la pili lilikuwa la mpira uliotulia.”
Naye kipa wa Tottenham, Hugo Lloris alikiri baadaye hakuona ni namna gani waamuzi wangebadili bao la Jesus na kutokuwa halali kupitia maamuzi ya VAR.
“Kusema kweli nilidhani ni bao. Kwa jinsi mwamuzi alivyochukua maamuzi ya awali ilikuwa asilimia 100 sahihi, halafu VAR ikafuta hilo bao na ni bahati mbaya kwa City. Kila mtu anaweza kuwa na tafsiri tofauti kuhusu hilo lakini tumefurahia kupata pointi moja. Lucas (Moura, mfungaji wa bao la kusawazisha) anastahili sifa nyingi.”
Naye Kocha wa Tottenham, Mauricio Pochettino anaamini msimu huu Tottenham itapata haki yake baada ya kulalamikia maamuzi ya Ligi Kuu ya England kwa muda mrefu msimu uliopita.
“Nilikuwa nakosoa sana siku za nyuma lakini sasa nitazikubali kanuni na katika siku za mbele pia kwa sababu najua matukio mengine yatakuwa dhidi yetu. Tulikuwa tumeudhika baada ya lile bao lakini baada ya kwenda VAR tukaona alikuwa amenawa. Ni hali ileile kama ilivyokuwa katika Ligi ya Mabingwa tulikuwa tumetolewa lakini ghafla tukaendelea. Ni kitu cha kushangaza inatokea katika uwanja huu huu na mechi za Tottenham,” alisema Pochettino.

Advertisement