Chilunda aamua kufunguka kurudi kucheza Bongo

Muktasari:

Mimi ni mchezaji wa Azam, kule nilienda kucheza kwa mkopo na muda wangu uliisha ndio maana nimerejea, acha kwanza nipambane na timu yangu na mengine yatajulikana

Dar es Salaam. Mshambuliaji Shaaban Idd Chilunda ameweka wazi kurejea kwake katika kikosi chake cha Azam FC, pamoja na kwamba bado ana ndoto ya kuondoka tena kucheza soka la kulipwa nje ya nchi.
Akizungumza baada ya mchezo wa Ngao ya Jamii juzi Jumamosi, alisema amerejea rasmi Azam lakini anaweza kuondoka tena kutokana na mipango iliyopo mbele yake.
“Mimi ni mchezaji wa Azam, kule nilienda kucheza kwa mkopo na muda wangu uliisha ndio maana nimerejea, acha kwanza nipambane na timu yangu na mengine yatajulikana,” alisema.
Kuhusu majaribio yake aliyokuwa anafanya Sweden, alisema yalienda vizuri na lolote linaweza kutokana na usajili bado haujafungwa nchini humo.
Aliongeza anaamini makosa ambayo yameonekana katika mchezo wao wa Ngao ya Jamii, yatasaidia kutoa mwanga kwenye mchezo wao wa marudiano kwenye Kombe la Shirikisho.
“Mchezo wa leo naamini umetoa taswira nzima ya nini tunafanya, mwalimu atafanyia kazi ili kuhakikisha tunafanya vizuri kwenye mchezo wetu unaokuja,” alisema chipukizi huyo aliyeitanguliza Azam kwa bao tamu la shuti kali katika kipigo cha 4-2 walichopewa na Simba kwenye mechi hiyo ya ufunguzi wa msimu mpya wa Ligi Kuu.