PSG yajitosa jumla kwa Dybala, Juventus yataka dau la kufuru

Monday August 19 2019

Mwanaspoti, Tanzania, Dybala azigonganisha, PSG, Juventus, Michezo, Mwanasport

 

Paris, Ufaransa. Paris Saint Germain (PSG), imeanzisha mazungumzo ya kumsajili mshambuliaji wa Juventus, Paulo Dybala katika usajili wa majira ya kiangazi.

Klabu hizo zimeanzisha mazungumzo na huenda zikafikia mwafaka wiki hii kabla ya dirisha la usajili wa Ulaya kufungwa Septemba 2.

Juventus inataka ilipwe Pauni73 milioni dau ambalo awali lilikataliwa na Manchester United.

Mkurugenzi wa Ufundi wa PSG, Leonardo, anatarajia kukamilisha usajili wa mchezaji huyo wa kimataifa wa Argentina.

Wakala wa Dybala, Jorge Antun, anatarajiwa kumalizana na Leonardo kabla ya dirisha la usajili wa majira ya kiangazi kufungwa.

Hata hivyo, dau hilo linaweza kuwa kikwazo kwa PSG kupata saini ya Dybala ambaye ujio wa Cristiano Ronaldo umemuweka njiapanda Juventus.

Advertisement

Ronaldo ameuteka ufalme wa Dybala tangu alipojiunga na Juventus akitokea Real Madrid.

Dybala hana namba kikosi cha kwanza na hayumo katika mpango wa kocha Mtaliano Maurizio Sarri.

Mchezaji huyo alikaribia kutua Man United, lakini alitaka dau kubwa la mshahara ambalo mashetani wekundu walikataa.

Tottenham Hotspurs ilikubali kutoa Pauni69 milioni kukamilisha usajili wa Dybala kabla ya mpango huo kuzimika ghafla

Advertisement