VIDEO: Simba kanyaga kanyaga, Msudani alamba ukwaju wa Azam

Muktasari:

Simba ikikutana kwa mara ya pili na Azam katika mechi ya michuano hiyo ya kuashiria ufunguzi wa msimu mpya wa Ligi Kuu Bara 2019-2020 na kushinda mabao 4-2, huku kiungo mpya kutoka Sudan akifanya mambo makubwa uwanjani akifunga mabao mawili, huku mechi hiyo ikichezeshwa na waamuzi sita.

Dar es Salaam. MNAHESABU lakini? Ndivyo walivyokuwa wakiimba mashabiki wa Simba wakati Shiboub Sharaf akitupia mabao kwenye Uwanja wa Taifa, Wekundu wa Msimbazi walipokuwa wakiiadhibu Azam katika mchezo wa Ngao ya Jamii.
Simba ikikutana kwa mara ya pili na Azam katika mechi ya michuano hiyo ya kuashiria ufunguzi wa msimu mpya wa Ligi Kuu Bara 2019-2020 na kushinda mabao 4-2, huku kiungo mpya kutoka Sudan akifanya mambo makubwa uwanjani akifunga mabao mawili, huku mechi hiyo ikichezeshwa na waamuzi sita.
Kiungo huyo mrefu alifunga bao la kwanza kwa kichwa baada ya mkwaju mkali wa Hassan Dilunga ‘HD’ kupanguliwa na kipa Razack Abarola naye kuuwahi na kuukwamisha wavuni, likiwa bao la kusawazisha katika dakika ya 16.
Azam inayonolewa na Kocha Etienne Ndayiragije mwenye rekodi ya unyonge mbele ya Wekundu wa Msimbazi tangu atue nchini mwaka 2016, ndio waliokuwa wa kwanza kupata bao dakika ya 13 kupitia kwa straika chipukizi Shaaban Chilunda.
Chilunda aliyekuwa akicheza soka la kulipwa Hispania kabla ya kurejea hivi karibuni alifunga bao tamu kwa kufyatua kombora la mwana ukome ambalo, lilimshinda maarifa kipa Beno Kakolanya na wakati mashabiki wachache wa Yanga wakishangilia bao hilo sambamba na wale wa Azam, ndipo Shiboub akawanyamazisha kwa bao la kusawazisha.
Tangu mapema mabeki wa Simba walionekana kukosa umakini wa kumdhibiti Chilunda aliyewakosa bao katika dakika ya saba, alipopaisha mpira akiwa yeye na Kakolanya aliyeonekana kukabiliana naye vyema na kumfanya apotee maboya.
Simba iliwachezesha kwa pamoja Pascal Wawa na Erasto Nyoni, huku pembeni Shomary Kapombe na Mohammed Hussein ‘Tshabalala’ walitulia baada ya kufungwa bao na Azam na waliposawazisha walizidi kuonyesha umahiri na kuwabana vilivyo wapinzani wao.
Ikiwa imewaanzisha wachezaji wanne wa kulipwa dhidi ya sita wa Azam, ilitawala mchezo na kuwakimbiza azam na katika dakika ya 22 walipata faulo iliyopigwa na Tshabalala na kuungwanishwa moja kwa moja na Shiboub akiwaacha wapinzani wao wakilaumiana.
Bao hilo tamu liliwafanya mashabiki wa Simba kulipuka na kuanza kuimba jina la kiungo huyo Shiboub... Shiboub... Shiboub.... mnahesabu lakini.
Kocha Patrick Aussems aliamua kumtoa John Bocco dakika chache baadaye baada ya nahodha huyo akionekana kuchechemea kutokana na kuchezewa vibaya na Frank Domayo na nafasi yake kuchukuliwa na Clatous Chama na hadi mapumziko matokeo yalikuwa 2-1.
Kipindi cha pili timu zote zilirudi kwa kasi na kufanya mabadiliko kadhaa, lakini ilionekana wazi Ndayiragije hajapata dawa ya kuizuia Simba kwani, Chama aliwanyanyua tena mashabiki wa Msimbazi kwa kufunga bao la tatu baada ya kuwahadaa mabeki wa Azam.
Chama alipokea mpira ulioguswa na beki wa Azam na katika dakika ya 56 kisha akawahadaa mabeki wa Azam na kukimbia na mpira na kuupenyeza pembeni kwa mbavu
za Abarola aliyetoka kumkabili na kuzidi kuwapa raha mashabiki wa Simba.
Dakika ya 78 Domayo aliipatia Azam bao la pili kwa shuti kali baada ya Obrey Chirwa aliyeingia kipindi cha pili kukimbia na mpira pembeni kisha kutoa krosi iliyounganishwa kwa shuti kali na kiungo huyo wa zamani wa Yanga akimuacha Kakolanya hana la kufanya.
Hata hivyo mtokea benchi Francis Kahata akichukua nafasi ya Dilunga alifunga bao la nne lililowakatisha tamaa Azam katika dakika ya 83 na mpaka mwamuzi wa pambano hilo, Elly Sasii anapuliza kipyenga cha mwisho, Simba walikuwa wababe kwa ushindi wa mabao 4-2.
Ushindi huo umeifanya Simba kutwaa taji hilo kwa mara ya tatu mfululizo na kufikia rekodi iliyowahi kuweka na Yanga mwaka 2013, 2014 na 2015, lakini pia wakilingana sasa kwa kutwaa taji hilo kwa mara ya tano tangu michuano ilipoasisiwa mwaka 2001.
Simba ilitwaa taji hilo pia katika mwaka 2011 na 2012 kisha kurudia tena 2017 na 2018 na Kocha Mkuu wa Simba, Aussems alisema amefurahi kupata matokeo hayo ikiwa ni taji lao la kwanza kwa msimu huu, lakini mechi hiyo anaitumia kwa maandalizi ya mchezo wao wa marudiano ya Ligi ya Mabingwa Afrika dhidi ya UD Songo ya Msumbiji.
Mfungaji wa mabao mawili ya Simba, Shiboub alisema anamshukuru Mungu kwa kuanza vyema msimu kwa kuifungia timu yake na pia kuwapa taji Wekundu wa Msimbazi na kuamini huo ni mwanzo mzuri na atapambana kufunga kila kwenye mechi.
Domayo na Chilunda kwa upande wao walieleza walicheza vizuri, lakini bahati haikuwa yao na wamekubali kwani soka ndivyo lilivyo na kusisitiza wanaenda kujipanga kwa ajili ya msimu mpya wa Ligi Kuu Bara 2019-2020 utakaonza wiki ijayo.
Vikosi vilipangwa hivi;
SIMBA: Kakolanya, Kapombe, Tshabalala, Nyoni, Wawa, Mkude, Dilunga/ Kahata, Shiboub/ Vieira, Kagere, Bocco/Chama, Kanda/Miraj
AZAM: Abarola, Wadada/Chirwa, Kangwa/Cabaye, Masai, Yakubu, Domayo, Mvuyekure, Sure Boy, Chilunda/Abdul, Djodi, Mahundi/ Hoza.