Mwalala atuliza akili aigeukia Al Ahly Shandy

Baada ya kuicharukia safu yake ya kati kwa kuwaangusha kwenye mkondo wa kwanza wa dimba la CAF CoCAF, confederation dhidi ya Al Ahly Shandy ya Sudan, kocha wa Bandari FC, Bernard Mwalala sasa katulia na kuyakusanya mawazo yake.

Timu hizi zitarudiana ugenini kule Sudan ndani ya wiki mbili zijazo baada ya kutoka sare tasa uwanjani Kasarani wikendi iliyopita.

Baada ya mchezo kuisha, kocha Mwalala aliwajia juu viungo wake akiwalaumu kwa kuwauza. Mwalala alisema middle yao ilikuwa imekufa na katika hilo ikashindwa kuwasambizia mipira mastraika wake ili waweze kumalizia.

Hata hivyo baada ya kutuliza jazba yake na kuyaweka mawazo yake sawa, Mwalala kawaonya wapinzani wake kwamba watarajie kuiona Bandari tofauti kabisa na ile waliyomenyana nayo Kasarani.

“Mwanzo hatukuwa na ufahamu wowote kuwahusu wapinzani wetu kama ilivyo sasa. Mpango wetu kule ugenini ni kusaka bao la mapema ili tuwape kazi ya ziada ya kufanya. Katika hilo nasi tujipange kuwakosesha amani,” Mwalala kafichua mpango wake.

Kocha huyo kasisitiza kuwa wana fursa nzuri ya kusonga mbele kwa sababu wapinzani wao hawakupata bao la ugenini, hivyo ndio watakaokuwa na presha kuliko wao.