Mambo matatu yaliyoziponza Simba, Yanga kimataifa

Tuesday August 13 2019

Tanzania, Mwanasport, Mwanaspoti, Mambo matatu, yaliyoziponza Simba, Yanga kimataifa

 

By Charles Abel

Dar es Salaam. Mambo matatu yamechangia kuziangusha timu sita zinazoiwakilisha Tanzania kwenye mashindano ya kimataifa katika mechi za kwanza za raundi ya awali zilizocheza mwishoni mwa wiki iliyomalizika juzi.
Wawakilishi hao sita ni Yanga na Simba za Tanzania Bara zinazoshiriki Ligi ya Mabingwa Afrika kama ilivyo kwa KMKM ya Zanzibar. Kombe la Shirikisho Afrika zipo KMC, Azam na Malindi ya Zanzibar.
Timu hizo sita zimeshindwa kupata matokeo mazuri kutokana na ubutu wa safu ya ushambuliaji, kukosekana kwa muunganiko bora wa kitimu pamoja na udhaifu wa safu za ulinzi na kujikuta zikikabiliwa na mlima mrefu wa kupanda katika mechi za marudiano ili ziweze kufuzu hatua inayofuata.
Hakuna timu hata moja kati ya hizo sita ambayo iliweza kupata ushindi, huku nne zikitoka sare na mbili zikipoteza.
Nuksi ilianza kwa KMKM iliyoanza kwa kuchapwa mabao 2-0 nyumbani na 1º de Agosto ya Angola, na kisha Simba ilitoka suluhu na UD Songo ya Msumbiji, matokeo ambayo yalipatikana pia kwenye mechi baina ya KMC na AS Kigali huku baadaye Yanga ikimaliza kwa sare ya bao 1-1 dhidi ya Township Rollers ya Msumbiji.
Wikiendi mbaya kwa wawakilishi wa Tanzania, iliendelea juzi Jumapili baada ya Azam FC kupokea kichapo cha bao 1-0 ugenini dhidi ya Fasil Kenema ya Ethiopia.
Hata hivyo, kukosa umakini, utulivu na ubutu wa safu za ushambuliaji kwa timu hizo kulichangia kuzigharimu.
Licha ya kila timu kutengeneza nafasi, washambuliaji walipoteza kutokana na kuchelewa kukaa kwenye nafasi sahihi, kushindwa kufanya uamuzi wa haraka ama kushambulia kwa pupa jambo lililochangia washindwe kufunga.
Na kwa kudhihirisha hilo, katika mechi sita za hatua ya awali ambayo timu hizo zimecheza, zimefunga bao moja tu ambalo lilipachikwa na Yanga katika sare ya 1-1 dhidi ya Rollers lililotokana na mkwaju wa penalti.
Simba, Azam, Malindi, KMKM na KMC zilishindwa kupata bao katika mechi hizo za kwanza.
Pamoja na hilo, timu zote hazikonyesha uelewano na kucheza kitimu na badala yake kundi kubwa la wachezaji kila mmoja alitaka kuonyesha uwezo binafsi jambo ambalo lilikuwa na faida kwa timu pinzani ambazo ziliamua kutumia mbinu ya kudhibiti wachezaji wachache walioonekana kucheza vyema.
“Wachezaji wangu hawakuonyesha uelewano mzuri jambo ambalo lilituweka kwenye wakati mgumu kupata matokeo lakini naamini nafasi ya kurekebisha hilo ipo na nimepanga kucheza mechi mbili kabla ya kurudiana nao ili tuzidi kujenga muunganiko.
“Naamini nafasi ya kupata ushindi ugenini bado ipo hivyo hakuna sababu kwa watu kukata tamaa, waendelee kuisapoti timu,” alisema Kocha wa Yanga,  Mwinyi Zahera.
Lakini pia baadhi ya wachezaji wanaocheza safu za ulinzi za timu hizo, walifanya makosa binafsi ya mara kwa mara ambayo yaliwapa faida washambuliaji wa timu pinzani kushambulia milango yao na pia hata kupachika mabao.
Udhaifu mkubwa katika safu ya ulinzi ulikuwa katika kuokoa mipira ya krosi na kuruhusu wapinzani kupenya kirahisi na kuingia kwenye lango lao.
Mfano wa mashambulizi hayo ni lile lililozaa bao la Rollers, ambapo mfungaji Phenyo Serameng alitumia udhaifu wa safu ya ulinzi ya Yanga iliyomruhusu kuingia katika eneo lao la hatari kwa urahisi.
Kocha wa Simba, Patrick Aussems alikiri timu yake haikuonyesha kiwango bora kama alivyotegemea na kuahidi kujipanga kwa mechi ya pili. “Kwa kiasi chake wachezaji wamepambana licha ya kukosa ushindi. Kuna mambo madogo ambayo hayajafanyiwa kazi, hivyo tunajipanga katika mchezo wa marudiano,” alifichua Aussems.
Matokeo hayo yanazilazimisha timu hizo sita kupata ushindi katika mechi za marudiano zitakazochezwa mwishoni mwa wiki ijayo ili zifuzu hatua ya kwanza.
Presha kubwa ipo kwa Yanga na KMKM ambazo zitamaliza ugenini zikihitaji kupata ushindi vinginevyo zitaaga mashindano hayo. Sare ya mabao kuanzia mabao 2-2 pia itaivusha Yanga huku ikitoka sare tasa italazimika kwenda kwenye mikwaju ya penalti ingawa kufungwa au sare ya bila kufungana itawatupa nje.
Azam itakayokuwa nyumbani nayo itapaswa kuibuka na ushindi wa zaidi ya mabao mawili na kutowaruhusu Fasil Kenema kuwafunga bao ili wasonge mbele, wakati Simba, KMC na Malindi, zenyewe zitafuzu kwa ushindi wowote ule ingawa sare ya mabao itazitupa nje.

Matokeo
Fasil Kenema     1-0     Azam
Yanga     1-1     Township
AS Kigali     0-0     KMC
UD Songo     0-0     Simba
KMKM     0-2      1de Agosto
Mogadishu City     0-0     Malindi

Advertisement