Mo Salah katoswa tuzo za Uefa

Saturday August 10 2019

 

SUPASTAA, Mohamed Salah amepigwa chini kwenye orodha ya mastaa wanaowania tuzo za Wachezaji Bora wa Ligi ya Mabingwa Ulaya, huku kwenye orodha hiyo kukiwa na wachezaji sita wa kutoka kwenye kikosi cha Liverpool.
Mo Salah alifunga bao la kwanza kwa mkwaju wa penalti wakati Liverpool walipoichapa Tottenham Hotspur 2-0 kwenye fainali ya Ligi ya Mabingwa Ulaya msimu uliopita, lakini hakujumuishwa kwenye orodha ya kusaka mchezaji bora wa kila nafasi na badala yake, nafasi ya fowadi ametajwa Sadio Mane kutoka kwenye kikosi hicho cha Anfield.
Mane anagombania tuzo ya mshambuliaji bora wa Ligi ya Mabingwa Ulaya sambamba na wakali Lionel Messi na Cristiano Ronaldo, huku wachezaji wengine wa Liverpool waliotajwa kuwania tuzo hiyo ni kipa Alisson Becker, mabeki Trent Alexander-Arnold na Virgil van Dijk na kiungo Jordan Henderson. Tuzo hizo hutolewa kwa mchezaji bora wa kila nafasi.
Spurs iliyopigwa kwenye mechi ya fainali, yenyewe imetoa wachezaji wawili, Hugo Lloris anayegombea kwenye nafasi ya kipa bora na Christian Eriksen kwenye mchuano wa kiungo bora.
Tuzo hizo za Ligi ya Mabingwa Ulaya kwa kila nafasi zinawashindanisha hawa, makipa Alisson Becker (Liverpool), Hugo Lloris (Tottenham), Marc-Andre ter Stegen (Barcelona). Mabeki ni Trent Alexander-Arnold (Liverpool), Matthijs de Ligt (Ajax, sasa Juventus ) na Virgil van Dijk (Liverpool) wakati kwenye viungo ni Frenkie de Jong (Ajax, sasa Barcelona); Christian Eriksen (Tottenham) na Jordan Henderson (Liverpool) huku washambuliaji ni Sadio Mane (Liverpool), Lionel Messi (Barcelona) na Cristiano Ronaldo (Juventus).

Advertisement