Tanzanite yaichapa Afrika Kusini yafuzu fainali Cosafa

Muktasari:

Tanzanite itawakabili Zambia katika mchezo wa fainali Jumapili kwenye uwanja wa Wolfson, huku Afrika Kusini wakicheza mchezo wa mshindi wa tatu na Zimbabwe, Jumamosi.

Dar es Salaam. Timu ya taifa ya Tanzania ya wanawake chini ya umri wa miaka 20 'Tanzanite', imetinga fainali ya Cosafa baada ya kuwafunga wenyeji wa mashindano hayo, Afrika Kusini kwa mabao 2-0 kwenye uwanja wa Gelvandale.

Tanzanite ilijipatia bao la kwanza dakika ya 18 kupitia kwa nahodha wake, Enekia aliyewazidi ujanja mabeki wa Afrika Kusini na kuachia shuti lililomshinda kipa na kujaa wavuni.

Dakika 12 baadae Tanzanite, inayonolewa na Bakari Shime walijipatia bao la pili la ushindi, kupitia kwa mshambuliaji wake hatari, Opa Clement.

Uimara wa safu ya ulinzi ya Tanzanite,uliwapa wakati mgumu Afrika Kusini ambao pamoja na  kulisakama lango la timu hiyo ya taifa ya Tanzania kipindi cha pili, walishindwa kupata bao la kufutia machozi.

Tanzanite ilitinga hatua ya nusu fainali ya Cosafa baada ya kuvuna pointi sita kutoka Kundi B kwa kuwafunga Botswana mabao 2-0 na Eswatini katika mchezo wa pili kwa  mabao 8-0 kabla ya kupoteza kwa Zambia mabao 2-1.

Katika mchezo wa nusu fainali ya pili, Zambia ambao walikuwa kundi moja na Tanzanite (B) nao waliibuka na ushindi wa bao 1-0 mbele ya Zimbabwe.

Kikosi kamili cha Tanzanite kilichoanza kwenye mchezo huo,kiliundwa na Tausi Abdallah, Ester Gindulya, Enekia Kasonga, Protasia Mbunda, Emeliana Mdimu, Janeth Christopher, Diana Msemwa, Eva  Wailes, Opa Clement, Aisha Mashaka, Irene Kisisa.