Gor Mahia kama kawa, kama dawa buda!

Muktasari:

Pollack ni kocha mwenye uzoefu wa soka la Afrika akiwa ametumika sana kule Ghana ambapo alikochi klabu mbili miamba Asante Kotoko na pia Berekum Chelsea.

Nairobi. KAMA Kawa, kama dawa, unaambiwa uongozi wa  Gor Mahia wala haujapaniki kufuatia kujizulu kwa kocha wao Hassan Oktay.
Wameshakuwepo katika hali hiyo mara nyingi na kama vile mazoea, tayari wameshaanza kumsaka kocha wa kumrithi Oktay.
Duru zimetuarifu kwamba uongozi ulishaanza zamani mchakato wao wa kumsaka atakayekuwa kocha wao wa saba tangu 2012.
Kulingana na taarifa hizo ni kwamba uongozi umeshatua tena kwa kocha Mwingereza Steven Pollack wanayemwinda kuja kuchukua mikoba yake Oktay.
Kocha Pollack anatarajiwa kutua nchini leo Alhamisi kwa ajili ya  kutia sahihi mkataba wake na Gor. Japo uteuzi huo unaonekana kama vile wa pupa, chanzo kimetueleza kuwa Gor walikuwa tayari wameshaanza mazungumzo na Pollack baada ya kocha Oktay kuanza kuwapiga na vipindi.
“Tunamtarajia kocha huo kutua nchini Alhamisi (leo) kutia saini mkataba wake na kisha anaweza akasafirio na timu kuelekea Burundi kwa ajili ya mchuano dhidi ya Aigle Noir,” chanzo hicho kutoka ndani ya Gor kilieleza.
Pollack ni kocha mwenye uzoefu wa soka la Afrika akiwa ametumika sana kule Ghana ambapo alikochi klabu mbili miamba Asante Kotoko na pia Berekum Chelsea.
Kocha msaidizi Patrick Odhiambo kasema wapo tayari kumkaribisha Pollack huku akimhakikishia kwamba ataikuta timu ikiwa vizuri tayari kwa kibarua cha Jumapili.
“Tupo kwenye shepu nzuri, nimeshuhudia mabadiliko makubwa sana, vijana wamejifua kweli kweli wengi wao wameboresha viwango vyao na tunacholenga ni kuanza kazi kwa kuandikisha ushindi ugenini,” Odhiambo kasema.