Kuumia kwa Kante shaka tupu Chelsea

Muktasari:

Kiungo huyo aliyejiunga na Chelsea mwaka 2016 akitokea Leicester City, ana rekodi ya kufunga mabao sita katika mechi 105 alizocheza ndani ya klabu hiyo.

London, England. Ng’olo Kante wa Chelsea, ana nafasi ndogo ya kuanza mechi za msimu mpya wa Ligi Kuu England baada ya kuumia goti.

Mchezaji huyo wa kimataifa wa Ufaransa amerejea nyumbani akitokea katika ziara ya maandalizi ya msimu mpya kwa ajili ya kupata matibabu ya kina.

Kocha Frank Lampard ana hofu ya kumkosa kiungo huyo katika mchezo wa kwanza wa ufunguzi wa Ligi Kuu England dhidi ya Manchester United.

Kante huenda akawa nje ya uwanja kwa wiki tatu, hivyo hawezi kuwahi mechi za kuanza msimu mpya.

Lampard alipanga kumtumia Kante katika mechi mbili za kirafiki nchini Japan, lakini sasa atalazimika kupangua kikosi.

Hii ni mara ya pili Kante kupata maumivu ya goti, mwishoni mwa msimu uliopita, alipata maumivu katika eneo hilo.

Kiungo huyo aliyejiunga na Chelsea mwaka 2016 akitokea Leicester City, ana rekodi ya kufunga mabao sita katika mechi 105 alizocheza ndani ya klabu hiyo.