Ujio wa Singano TP Mazembe wampa mzuka Ambokile

Muktasari:

Kitendo cha Ramadhan Singano kusaini TP Mazembe, kimempa mzuka Eliud Ambokile kujiamini kwa kuwa na mtu wa kutoka nyumbani kwao Mtanzania.

Dar es Salaam. Mshambuliaji Eliud Ambokile amesema kitendo cha Ramadhan Singano kujiunga na TP Mazembe kinampa faraja na kujiamini watafanya kitu cha kuacha historia ndani ya timu hiyo.

Ambokile aliyetangulia kujiunga na TP Mazembe kabla ya Singano kusaini mkataba wa kuitumikia klabu hiyo hiyo.

Alisema licha ya kwamba alipata marafiki wa kushirikiana nao kwenye mambo mbalimbali, alidai ni tofauti na kucheza timu moja na Mtanzania mwenzake Singano.

"Tupo wote muda mwingi, tunatiana moyo jinsi ya kupambana kuonyesha vipaji vyetu dhidi ya wenyeji wa Congo na wengine waliosajiliwa nje ya hapa.

"Kwanza kikubwa ambacho nimejifunza kwenye timu hii ni ushindani wa mazoezi huku hakuna kusukumwa yaani kila mchezaji anajua wajibu wake kikamilifu kabla ya kocha kuanza kupewa maelekezo yake.

"Nidhamu ni kitu kinachozingatiwa halafu tumekutana na wachezaji ambao wana ndoto za kufika mbali zaidi, hilo linatupa nguvu ya kupambana zaidi, naamini tutafanya kitu cha tofauti kitakacholeta sifa Tanzania.

"Kuna wakati wakituona tupo na Singano, baadhi ya wachezaji wanatuambia tujitume tuwe kama walivyokuwa Mbwana Samatta na Thomas Ulimwengu, mengi tunaendelea kujifunza kwa kweli," alisema.