VIDEO: Kisa CAF: Kocha wa Simba mapema alia ratiba ngumu

Muktasari:

Ratiba hiyo ya CAF imetibua kalenda ya Simba Day pamoja ratiba ya mechi za Ligi Kuu Bara ambazo Simba inatakiwa kucheza mapema hivyo italazimika kubadilishwa.

Afrika Kusini. Kocha wa Simba, Patrick Aussems amelalamikia ratiba ya mwanzo wa msimu itakuwa ngumu kwake kwa sababu imekwenda tofauti na mipango yake.

Kauli ya kocha huyo wa Simba inakuja baada ya Shirikisho la Soka Afrika (CAF) kutoa ratiba ya mechi za awali za Ligi ya Mabingwa jana na Simba ikitakiwa kucheza mechi ya awali Agosti 9-11.

Simba itaanza ugenini dhidi UD Songo ya Msumbiji katika mechi itakayochezwa kati ya Agosti 9-11 na marudiano itakuwa kati ya Agosti 23-25, 2019.

Ratiba hiyo ya CAF imetibua kalenda ya Simba Day pamoja ratiba ya mechi za Ligi Kuu Bara ambazo Simba inatakiwa kucheza mapema hivyo italazimika kubadilishwa.

Akizungumzia suala hilo kocha Aussems alisema alitarajia mechi hizo zitaanzwa kuchezwa Septemba, lakini imekuwa kinyume.

"Natakiwa kufanya kazi ya ziada kutokana na ratiba hiyo. Baadhi ya programu nimeanza kubadilisha ratiba ya mazoezi ili kujaribu kwenda na wakati,"alisema Aussems.

Katika mazoezi yake leo Jumatatu, Aussems alitumia muda mwingi kuwafanyisha wachezaji mazoezi ya nguvu ambapo walikimbia na kucheza kwenye koni.

Simba inaendelea na mazoezi nchini Afrika Kusini kwa ajili ya kujiandaa na mechi za Ligi Kuu na mashindano ya kimataifa.

Katika Ligi ya Mabingwa Afrika, endapo Simba itashinda mechi yake dhidi ya UD Songo na kusonga mbele na kucheza dhidi ya mshindi wa mechi ya Big Bullets na FC Platinum kati ya Septemba 13-15, 2019 na marudiano Septemba 27-29, 2019.

Katika ratiba hiyo Yanga itaanzia nyumbani kwa kucheza dhidi ya Township Rollers timu waliyokutana nayo mwaka 2018 katika michuano hiyo na Vijana wa Jangwani kutolewa kwa kufungwa jumla ya mabao 2-1, ikilala nyumbani kwa bao hizo na kwenda kutoka suluhu ugenini.

Mshindi wa Yanga na Township Rollers atafuzu kwa raundi ya pili na kucheza na mshindi wa mechi kati ya Green Mamba ya eSwatini au Zesco United ya Zambia. Mshindi wa mechi hizo za pili inafuzu moja kwa moja kwa hatua ya makundi ya mashindano.

Katika Kombe la Shirikisho Afrika, mabingwa wa Kombe la FA, Azam itaanza ugenini dhidi ya Fasil Kenema ya Ethiopia kati ya Agosti 9-11, 2019.

Mshindi wa Azam dhidi ya Fasil Kenema atacheza na mshindi wa mechi kati ya Triangle United (Zimbabwe) dhidi ya Rukinzo (Burundi) katika raundi ya pili.

KMC inashiriki kwa mara ya kwanza mashindano hayo ikiwa chini ya kocha Jackson Mayanja itakuwa nyumbani kuikaribisha AS Kigali (Rwanda) anayoichezea Haruna Niyonzima aliyeachwa na Simba msimu huu.

Mshindi wa KMC na AS Kigali atacheza na mshindi wa mechi ya Proline (Uganda) dhidi ya Masters Security (Malawi)